Anayesema Nawe Ana Roho Gani Nyuma yake?
Ezekieli 2:1-2
Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe. Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.
Nataka tuyaangalie maneno hayo niliyonukuu hapo kwa pamoja na kwa undani kabisa.
Ukiangalia kwa makini mstari wa kwanza, hasa maneno yafuatayo "Akaniambia, Mwanadamu, simama"
Halafu tena ukaangalia kwa umakini na mstari wa pili "aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha;"
Utagundua muunganiko wa moja kwa moja wa maneno na roho au nguvu fulani kusababisha hayo maneno yatokee au yafanyike.
Sasa, hapa aliyesema na Ezekieli ni Mungu, kwa hiyo, roho iliyomuingia Ezekiel ilikiwa ni Roho wa Mungu nyuma ya yale maneno ya Mungu.
Mungu akasema na Ezekieli "Mwanadamu simama", Roho ikamuingia Ezekieli IKAMSIMAMISHA.
Ezekiel alisimamishwa na Roho iliyomuingia, hakusimama kwa nguvu zake na hiari yake pekee, kuna nguvu tokea nje (external force) ilimuingia kupitia maneno, ikamsukuma, ikamuhimiza kusimama.
Inawezekana kabisa hakuwa anataka kusimama wala hakuwa na mpango wa kusimama lakini mara tu baada ya kusikiliza yale maneno akaanza kusikia msukumo wa kusimama na akasimama.
Mimi naona hapa kuna fundisho au funzo kubwa sana.
Kwenye kila maneno kuna roho nyuma yake kuyafuatilia hayo maneno.
Ninaposema roho nyuma ya maneno ninamaanisha kuna nguvu fulani nyuma ya hayo maneno ambayo lengo lake ni kuyafanya yale maneno yatokee au yatimie kwa anayesikiliza.
Hii ni kanuni kabisa ya ulimwengu wa roho.
Unajua, moja ya namna ya kufanya kilicho katika ulimwengu wa roho kiwe halisi kwenye ulimwengu wa mwili ni kwa kutumia MANENO AU MATAMSHI. Na kanuni hiyo ndio Mungu aliitumia katika uumbaji.
Mwanzo 1:3,6 “Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji.”
Kimsingi, kila unachosikiliza kina roho nyuma yake ambayo kazi yake ni kufuatilia hayo maneno yaliyosemwa. Nimesema hivi kwa sababu, kilichokufa hakiwezi kuongea, kinachoongea kina roho ndani yake.
Ninachotaka tuelewe ni kwamba, mtu akifa hawezi kuongea, anayeongea ni aliye hai, na aliye hai anayo roho ndani yake, kwa hiyo kinachoongea ndani ya mtu sio mdomo tu bali ni ile roho ya mtu iliyo ndani yake, kwa hiyo yale maneno anayoongea ni roho au yanabeba roho ya anayeongea.
Yesu akasema, Yohana 6:63 "Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima."
Hii roho na uzima katika maneno ya Yesu yalitokana na uzima uliokuwa ndani ya roho ya Yesu.
Kama kuna maneno ambayo ni roho na uzima basi tuwe na uhakika kuna maneno ambayo ni roho na mauti au roho na uharibifu au ni roho ya mauti. Yanakuja kuharibu na kuua hatma zetu.
Kwenye ulimwengu wa roho kuna pande mbili tu, kuna ulimwengu wa nuru na ulimwengu wa giza. Kuna ufalme wa Mungu na ufalme wa giza, hii ina maana kwamba hata roho nyuma ya maneno zina pande mbili, upande wa nuru na wa giza. Kila mwanadamu anaangukia upande mmoja kati ya mbili, wana wa nuru (ufalme wa Mungu) na wana wa giza (Ufalme wa Shetani) hakuna wa katikati (neutral).
Swali la kujiuliza, unachosikiliza kina roho gani nyuma yake?
"Akaniambia, Mwanadamu, simama.... Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha;"
Unachosikiliza kina ujumbe au maagizo gani? Hiyo roho ikikuingia itakufanya nini? Itakusimamisha au itakuangusha? Itakusimamisha katika nini au katika kufanya nini?
Ujumbe wa Ezekiel ulikuwa “Mwanadamu Simama" roho ikamuingia IKAMSIMAMISHA.
Unayemsikiliza ana roho gani? Na anachosema kimebeba nini kwa ajili yako?
Kimsingi hapa swala la kwanza sio ujumbe wa maneno bali ni roho ya mtoa (mbeba) ujumbe.
Kama mtoa ujumbe ni mchafu, hata akitoa maneno mazuri yatabeba roho yake CHAFU.
Ni sawa na mfano wa maji, usafi wa maji hauko kwenye "rangi" au "weupe" wa maji bali uko kwenye chanzo cha maji... Maji hata yakiwa "meupe" vipi, kama yametoka chanzo kibovu hayafai kwa kunywa.
Wale tunaofahamu choo cha kukaa tunaweza tukaelewa vizuri mfano huu, ukiingia kwenye choo cha kukaa ambacho ni kisafi sana, utaona ndani yake kuna maji "meupe" au masafi.Lakini pamoja na kwamba ni "meupe", hayafai kabisa kwa kunywa sio kwa sababu yanaonekana machafu lakini ni kwa sababu ya chanzo chake.
Mtu mchafu hata akiongea maneno masafi, maneno yake hayafai kwa sababu yametoka katika chanzo kichafu.
Luka 6:44 “kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu.”
Ukiona mchongoma unatoa zabibu hiyo zabibu usiirukie, haifai kuliwa, ni zabibu feki
Sasa anza kujiuliza.; Unamsikiliza sana nani? Na ana roho gani ndani yake?
Unasikiliza sana nini? Watu gani unawasikiliza sana? Miziki gani? Tamthilia gani? filamu gani?
Unajua roho gani iko nyuma ya hao watu? Hao ambao unaangalia tamthilia zao na unasemea hiyo tamthilia inafundisha, huyo anayekufundisha ana roho gani nyuma yake?
Huo mziki unaosikiliza eti kwa sababu umetaja "haleluya" au eti umetaja "Mungu", je huyo aliyetaja Mungu anaye Mungu wa kweli?
Hivi umewahi kujiuliza kwa nini sasa hivi uzinzi umekuwa janga sio tu kwa dunia bali hata kwa kanisa? Sababu kubwa ni kanuni hii ya roho nyuma ya maneno.
Angalia, miziki karibu yote inazungumzia mapenzi, tamthilia karibu zote, filamu karibu zote zinazungumzia mapenzi na uzinzi; na ukiangalia MAISHA YA WANAMZIKI NA WASANII WENGI YAMEJAA UZINZI, kwa hiyo kuna roho ya uzinzi nyuma ya watu na maneno wanayowakilisha kupitia filamu, filamu, tamthilia na miziki na roho hizo huwaingia wanaowafuatilia na kusababisha janga la uzinzi kila mahali.
Umewahi kujiuliza huyo mkaka au mdada, mwanaume au mwanamke uliye mpa nafasi kumsikiliza sana maneno yake au ushawishi wake, je ana roho gani nyuma yake?
Hiyo roho ikikuingia itakusimamisha au itakuangusha au imeshakuangusha?
Wengine ni mashahidi, baada ya kuanza kusikiliza sana watu fulani tumeanza kuona tumebadilika, kuna hali fulani imetuingia, kuna vijitabia fulani hatukuwa navyo na vimeanza kututesa.
HAKUNAGA MANENO MATUPU.
Kabla ya kuamua kusikiliza maneno hakikisha uko tayari roho iliyo nyuma ya hayo maneno KUKUINGIA, kama hauko tayari USIYASIKILIZE.
Waamuzi 16:16 “Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.”
Kilichomponza Samson ni kuendelea kusikiliza maneno ya ubembelezi ya Delila.
Samson alipoendelea kusikiliza maneno ya Delila, roho yake ikadhikika au ikadhoofishwa na nguvu ya maneno, mpaka ikafa, na hapo ndipo akajikuta anakaribisha mauti ya kile Mungu alichoweka ndani yake na mauti yake binafsi.
Unapofanya maamuzi ya kumsikiliza mtu, kaa ukijua fika umefungua mlango/ umeruhusu roho nyuma ya huyo mtu ikuingie kupitia maneno yake.
Je, anayesema nawe, au unayesoma jumbe zake au unayesikiliza nyimbo zake, ana roho gani nyuma yake?
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
+255754711247
Mwl. Francis Langula
Author