Text

Bado Kitambo Kidogo Sana, Yeye Ajaye Atakuja

1 views 1 day ago

Waebrania 10:37

Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.

Neno la Mungu linasema bado kitambo kidogo sana Yeye ajaye (yaani Yesu) atakuja, wala hatakawia.

Huu ndio ukweli tulionao sasa! Na hata dalili zinaonyesha wazi kwamba Yesu yuko mlangoni.

Yaani Neno linaweka wazi kwamba tufanye kila jambo tukitambua kwamba hatuna muda hapa duniani.

Linahimiza kwamba tusijisahau, tuwe tayari muda wowote Yeye ajaye atakuja.

Kuna mambo yalikuwa yanazungumziwa zamani kuhusu kurudi kwa Yesu ambayo tulikuwa hatupati picha yatatokeaje lakini sasa hivi TUNAYAONA KWA MACHO.

Ujio wa Yesu si tu kwa dalili za nje bali hata kwa dalili za mioyoni kwa wale ambao wako makini (sensitive) kwa Roho Mtakatifu.

Kuna namna Roho zetu zinachangamka na kuwa na hali fulani ya kujiweka tayari kwa safari.

Kuna namna shauku ya Rohoni ya kumuona Yesu mawinguni inaongezeka siku hata siku.

Kuna namna dunia inazidi kupoteza ladha (taste) kwa kadiri siku zinavyosogea.

Kuna ishara zinatokea ndani ya kila roho ambayo ina Roho Mtakatifu ndani yake.

Roho Mtakatifu mwenyewe analiandaa kanisa lake kwa ujio wa Yesu.

Kwa wale wahubiri, kuna namna Roho Mtakatifu analeta jumbe za kuwaandaa watu kwa ajili ya kuondoka (take off).

Analeta jumbe za kuwaonya watu wasiishi kama wamefika duniani bali kama wapitaji.

Jumbe za kuwaonya watu wasijisahau, kuwaonya watu wailinde na kuitunza imani kwa sababu moja ya kitu adui anatafuta siku hizi za mwisho ni IMANI YA WATAKATIFU.

Luka 21:28 Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.

Mathayo 24:32-33 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.

Lakini, kwa upande wa pili, wakati Roho Mtakatifu akisisitiza muda UMEISHA, Shetani naye yuko busy kuwasahaulisha watu juu ya jambo hilohilo na kuwaonyesha kwamba mambo yako vile vile tu.

Shetani yuko busy kuonyesha ukawaida wa mabadiliko tunayoyaona, watu waone ni mabadiliko ya kawaida na si kitu kinahusiana na siku za mwisho.

Anaonyesha watu kuwa Matetesi ya vita kila mahali ni mambo ya kawaida... Maasi kuongezeka ni kawaida,

Mathayo 24:6,12 Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa.

Teknolojia kuongezeka kwa kasi kubwa ni hali ya kawaida.

Danieli 12:4 Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.”

Dunia kuungana kuwa kitu kimoja ni kawaida... Harakati za kuwa na dini moja ni kawaida... Harakati za kuwasajiri wanadamu kwenye database moja ni kawaida...

Shetani anaonyesha ukawaida kabisa wa Harakati za kuunda mifumo ya kisayansi ambayo itaingilia na kuathiri uhuru wa KUSAFIRI, KUNUNUA NA KUUZA, KUKUSANYIKA, KUABUDU nk.

Ufunuo wa Yohana 13:17-18 tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.

Kuna maandiko yamekuwa kama yamesahaulika kwa watu, na tunasahau kabisa mengi yanayotokea yanaandaa utendaji wa mpinga Kristo.

Kila sauti inayokuambia bado kuna muda wa kuendelea kukaa duniani kwa hiyo ishi vyovyote hiyo si sauti ya Mungu.

Hiyo hali inayokuonyesha hakuna uharaka wa kurekebisha maisha yako sio sauti ya Mungu ni ya shetani kabisa.

Hiyo hali inakuambia haina shida HII DHAMBI UTAISHUGHULIKIA HATA KESHO HAKUNA HARAKA YOYOTE, hiyo nakuhakikishia SIO SAUTI YA MUNGU, kwa sababu NENO LINASEMA YU MLANGONI.

Hiyo sauti inayokuambia ENDELEA TU NA HAYO MAHUSIANO AMBAYO UNAJUA KABISA YANAKUTENGA NA MUNGU WAKO, hiyo sio sauti ya Mungu.

Hiyo inayokuambia ENDELEA NA HAYO MAISHA UTATUBU KESHO AU UTAOKOKA KESHO MUDA BADO UPO, HIYO SI SAUTI YA MUNGU KWA SABABU YESU YU MLANGONI.

Ufunuo wa Yohana 3:11Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.

Yesu anakuja upesi, usikubali MTU (MAHUSIANO) YOYOTE akukoseshe.

Ufunuo wa Yohana 22:7 Na tazama, naja upesi; heri yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.

Yesu anakuja upesi, hakikisha unashika na kuliishi Neno la Mungu kwa nguvu zako zote.

Ufunuo wa Yohana 22:12 Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

Yesu anakuja upesi, HAKIKISHA UNA TUMIKA MUNGU KWA NGUVU ZAKO ZOTE NA KWA BIDII.

Ufunuo wa Yohana 22:20 Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu.

Yesu anakuja Upesi, Je unao ujasiri wa kusema "Amina; na uje, Bwana Yesu.?

Kama unaona ndani yako hauna huo ujasiri na huo utayari TAFADHALI WAKATI NDIO SASA WA KUFANYA MAAMUZI NA KUHAKIKISHA UNAJIWEKA TAYARI.

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

#Umebarikiwa
~Na Mwl. Francis Langula 

+255754711247

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!