Text

Chagua Kuwa Mzima, Chagua Kupona

1 views 1 day ago

Kumbukumbu la Torati 30:19Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; BASI CHAGUA UZIMA, ili uwe hai, wewe na uzao wako;
Nakumbuka kuna wakati, zaidi ya mwaka umepita, nilipata shambulizi la afya nikaumwa kiasi ambacho wanafamilia na baadhi ya watu nje wakafahamu kwamba nina shida ya afya. 
Kabla ya hapo imewahi kutokea mara kadhaa ninapata dalili kali za kuumwa au ninahisi kuumwa kabisa lakini ninamuamini Mungu na ananiponya kabisa bila mtu yeyote, hata wa karibu, kugundua hali niliyokuwa nayo; kwa sababu hata mara moja nilikiwa sikubali ugonjwa ukaathiri ratiba zangu za kila siku, lakini mara hii ilikuja kwa kiwango ambacho kiliathiri kabisa mwili wangu, ratiba zangu na haikuwezekana watu wasijue. 
Sasa, baada ya watu kufahamu nina changamoto, kuna namna wakawa wananijulia hali mara kwa mara kwa simu na meseji na kwa sababu wanajua nikawa mara zote nawaelezea kinachoendelea mwilini mwangu; mfano mtu akiuliza namwambia leo kwa kweli nimeshindwa kabisa kula, kichwa kinaniuma sana, nimekuwa na homa kali usiku wote, mwili wote una maumivu, sijainuka kitandani tangu asubuhi na mengine mengi na kwa kweli nilikuwa nawaambia kinachoendelea mwilini mwangu. 
Nakumbuka moja ya kitu ule ugonjwa ulianza kufanikiwa kwangu ni kuvuruga kabisa ratiba yangu, yaani nikawa siwezi kuamka tena kuomba, siwezi kabisa kusoma vitabu, kusikiliza mafundisho, siwezi kufunga, ilikuwa siku nzima nashinda nimelala; ambacho haukuweza kuvuruga ni ratiba ya kuhubiri, yaani hata kama nina hali gani ilikuwa ikifika saa natakiwa kusimama kuhubiri nilijilazimisha na kuhubiri na nikiwa nahubiri hakuna aliyeweza kuhisi kama ninaumwa, lakini baada ya kutoka madhabahuni nilikuwa napata shida sana. 
Hali hii ilikaa katika mwili wangu kama wiki mbili hivi na siku zote hizo nilikuwa nawapa taarifa wanaonijulia hali kwa kuwaambia uhalisia wa mwili wangu, na japo nilikuwa Namuamini Mungu kuniponya kwa muda wote huo lakini kwa kweli sikuwa na nafuu yoyote ila nilikuwa nikiona kama kila siku hali inakuwa mbaya. 
Nakumbuka usiku mmoja nikaamka kati kati ya usiku, Roho Mtakatifu akaniletea ndani yangu Neno hilo nililonukuu hapo juu, nikalitafuta na kulisoma. Wakati nalisoma akanionyesha kitu ambacho sikuwahi kukiwaza kabla japo Neno hilo nilikuwa nalifahamu sana. 
Maneno Yafuatayo kwenye andiko hilo yalikuja kwa nguvu ndani yangu
Kumbukumbu la Torati 30:19
... nimekuwekea mbele yako uzima na mauti,... BASI CHAGUA UZIMA, ILI UWE HAI, WEWE NA UZAO WAKO;
Nikaanza kuona, mbele yangu nina UZIMA na UGONJWA, na Mungu amenipa fursa ya KUCHAGUA na ananieleza kabisa NINI CHA KUCHAGUA, kwamba NICHAGUE UZIMA ILI NIWE HAI. 
Nikasema moyoni mwangu, kumbe NINAWEZA KUCHAGUA UZIMA. 
Nikawaza, nimekuwa namwamini Mungu aniponye kwa wiki zaidi ya mbili sasa na kila siku naona sipati nafuu, nikajisemea "SASA NATAKIWA KUFANYA MAAMUZI YA KILE NINACHOKITAKA."
Mungu amenipa wajibu kwenye swala la uzima na afya yangu, ameliweka kwenye utashi wangu KUCHAGUA NINACHOTAKA. 
Usiku ule ule nikaamua kuchagua ninachotaka... Nikasema "NINACHAGUA KUWA MZIMA"... NIKAONGEZEA NIKASEMA "NIMEAMUA KUWA MZIMA, NIMEAMUA KUPONA."
Kuanzia asubuhi iliyofuata, kila aliyekuwa ananiuliza unaendeleaje nilikuwa nampa jibu moja tu, "NIMEAMUA KUWA MZIMA, NIMEAMUA KUPONA" ambaye alikuwa anauliza zaidi nikawa nanukuu hilo andiko na namsisitizia kwamba "NIMEAMUA KUPONA."
Na tangu siku hiyo, sikuelezea tena ninachohisi ndani ya mwili wangu wala sikukipa tena umakini (attention); nilichokuwa najiambia, "NIMECHAGUA UZIMA NA NIMEAMUA KUPONA". 
Lakini jambo la pili ambalo nilifanya, NILIAMUA KUANZA KUENDELEA NA RATIBA YANGU KAMA MTU AMBAYE HAUMWI, NIKAANZA RATIBA KAMA MZIMA NA SIO MGONJWA.
Yaani, nikafanya maamuzi ya KUENDELEA NA RATIBA YANGU YA MAOMBI BILA KUJALI NAJISIKIAJE, nikaanza kuamka kuomba, nikasema siachi kuamka kama nikishindwa basi nishindwe NIKIWA NIMEPIGA MAGOTI NAOMBA NA SIO NIKIWA KITANDANI. 
Lakini pia nikaamua kuendelea na RATIBA YA MIFUNGO, KUSOMA NENO, KUSIKILIZA MAFUNIDSHO nk BILA KUJALI ninavyojisikia. 
Kwa siku kama tatu za mwanzo, tangu nimefanya maamuzi hayo, kwa kweli haikuwa rahisi, nilikuwa nafanya vyote kwa kujilazimisha sana na kuulazimisha mwili, lakini baada ya hapo NILIANZA KUFURAHIA NILICHOKICHAGUA KATIKA MWILI WANGU. 
Nilianza kusikia Mabadiliko ya haraka sana na NIKAPONA KABISA. 
Nikaona uhalisia na Nguvu ya KUCHAGUA. Kwa kweli NILIPATA NILICHOCHAGUA. 
Nikagundua kwamba kumbe wakati mwingine hatupati haki zetu (ikiwemo haki ya afya na uponyaji) kwa sababu hatufanyi maamuzi thabiti na kuyasimamia hayo maamuzi na uchaguzi wetu, KUCHAGUA UZIMA. 
Ninakumbuka habari ya yule mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka 12. Alipona siku ALIPOAMUA KUPONA na alipona KWA NAMNA ALIYOAMUA KUPONA. 
Mathayo 9:21 Kwa maana alisema moyoni mwake, NIKIGUSA TU upindo wa vazi lake NITAPONA.
Kabla ya kupona alisema moyoni mwake, NITAPONA KWA KUGUSA PINDO, NA NITAPONA MUDA NITAKAOGUSA PINDO LA YESU. Alichagua kuwa MZIMA. Aliamua kuanzia hapa ndio mwisho wa mimi kuwa mgonjwa na mwanzo wa mimi kuwa mzima. 
Aliamua kuweka msitari wa mwisho wa kuwa mgonjwa. 
Neno la Mungu ni kweli na halisi kwa kila ambaye ataamua kulifanyia kazi, hata wewe unayesoma ujumbe huu, unaweza UKAFANYA MAAMUZI NA KUCHAGUA KUWA MZIMA. 
CHAGUA UZIMA, NA AMUA KUWA MZIMA baada ya hapo USIISHI TENA KAMA MGONJWA KWA SABABU WEWE SIO MGONJWA BALI NI MZIMA. 
Fikiri kama mzima sababu wewe ni mzima, ongea kama mzima sababu wewe ni mzima, tenda kama mzima sababu wewe ni mzima.
Mathayo 8:17 Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.
Yesu alitwaa udhaifu, alichukua magonjwa yetu.
Kama alitwaa udhaifu wangu, mimi sio dhaifu, kama alichukua MAGONJWA YANGU mimi sio mgonjwa. Haiwezekani yeye atwae na mimi niwe nayo. Kama yeye anayo mimi sina. Kama yeye amechukua mimi sina. 
Mimi sina udhaifu wala sina ugonjwa kwa sababu anao Yesu. 
Mimi nimechagua KUWA MZIMA, MIMI NIMECHAGUA KUPONA, MIMI NIMECHAGUA KUISHI.
Huu ni mtihani ambao una majibu mawili, Uzima na Ugonjwa, na Mungu ameshatupatia jibu sahihi kwamba "BASI CHAGUA UZIMA, ili uwe hai, wewe na uzao wako;"
CHAGUA UZIMA NA UPOKEE UZIMA, CHAGUA KUPONA NA UPOKEE UPONYAJI KWA JINA LA YESU. 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa

~Na Mwl. Francis M. Langula

+255754711247

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!