Text

Dhambi ya Kiburi - Sehemu ya 2

1 views 1 day ago

1 YOH. 2:16

Maana KILA KILICHOMO DUNIANI, yaani, TAMAA YA MWILI, na TAMAA YA MACHO, na KIBURI CHA UZIMA, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

Andiko hilo nililonukuu limeweka wazi kabisa kwamba, HUMU DUNIANI tunapoishi, kuna maadui zetu wakubwa watatu, na maadamu maadui hao wapo duniani na sisi tunaishi Duniani, ni vizuri kufahamu kwamba siku zote tunapoishi wataendelea kujaribu kutufuatilia.

Maadui hao wakubwa ni:-

1. Tamaa ya Mwili

2. Tamaa ya Macho

3. Kiburi cha Uzima

Ni lazima kufanya maamuzi ya dhati kuwashinda hawa maadui kila siku, nasisitiza, KILA SIKU.

Dunia na Shetani ataendelea kuwatumia hawa maadui kutufuatilia mpaka siku tunaondoka duniani.

LEO, KWENYE TAFAKARI HII, NITAMUONGELEA ADUI MMOJA TU KATI YA HAO, NAYE NI KIBURI CHA UZIMA (PRIDE OF LIFE).

Kwa lugha rahisi anaposema KIBURI CHA UZIMA, ni KIBURI CHA MAISHA au KIBURI kwa sababu ya VILE ALIVYONAVYO MTU au VILE ALIVYO.

Kwa sababu dhambi hii ya KIBURI ndio ILIMUANGUSHA LUSIFA, kwa hiyo, anaweza kuitumia vizuri sana kututafuta nayo sababu ANA UZOEFU NAYO.

Tatizo la kiburi ni kwamba, UKIFANYA JAMBO ZURI, shetani atataka kutumia hilohilo, na UKIFANYA JAMBO BAYA pia shetani hutaka kutumia hilihilo kukuletea KIBURI. Yaani anaweza kuingilia mlango wowote, wa MAZURI au wa MABAYA anayofanya mtu.

Kimsingi, Shetani akigundua unafanya JAMBO ZURI, mbinu ya kwanza anayotumia ni KUKUZUIA USIENDELEE NALO; lakini akishindwa kukuzuia, mbinu ya pili ni KUKUFANYA UWE NA KIBURI NALO.

Mtaji anaotumia shetani kumjaribu mtu kwa DHAMBI YA KIBURI, hautoki nje ya mtu bali NI KILE ALICHO NACHO MTU NDANI YAKE au VILE ALIVYO.

Linapokuja swala la KIBURI, SHETANI mara nyingi HUTUMIA KIZURI ALICHO NACHO MTU, kwa mbinu kuu tatu:-

1) Kumzuia mtu asiendelee na hicho kizuri

2)Akishindwa kukizuia, Anakikuza hicho KIZURI ndani ya mtu kuliko uhalisia wake,

3) Anamfanya mtu aanze kujilinganisha na wengine, ili ajione yeye ni zaidi yao. Ajione yeye ni maalum (special) sana kuliko wengine.

Neno la Mungu linasema katika Mithali 13:10

Kiburi huleta mashindano tu; Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.

Shetani hukuletea aibu na woga ndani yako kufanya jambo zuri, ukiushinda woga na aibu na kufanikiwa, hutumia mafanikio yako na kufanya kwako vizuri kukuletea KIBURI.

Ngoja nieleze kidogo hapa maana ni muhimu sana kuelewa;

Shetani akiona UNAFANYA AU UNALO JAMBO ZURI sana, atajaribu kukuzuia usiendelee na HILO ZURI [Kama hicho kizuri kinazuilika], akishindwa ATAKUFANYA UJIONE WEWE UNAFANYA JAMBO ZURI [AU WEWE MZURI] SANA kuliko uhalisia wake, kisha atakufanya UJIONE WEWE UNAFANYA VIZURI KULIKO wengine WOTE kwa hiyo wewe ni wa pekee na UMEWAZIDI WENGINE WOTE, kwa hiyo BILA WEWE MAMBO HAYATAENDA. NA KWA KUFANYA HIVYO ATAHAKIKISHA HAUUONI MCHANGO WA WENGINE NA KUINUA KIBURI ndani yako.

Ukiwa MZURI shetani atataka kutumia uzuri wako, Ukiwa muombaji au mfungaji mzuri, SHETANI atataka kutumia uombaji na ufungaji wako, vilevile ukiwa muimbaji mzuri, au Mwalimu mzuri, au muhubiri mzuri, mfanya biashara mzuri, ukiwa na vipawa vizuri, nyumba nzuri, magari, akili nk HICHO KIZURI CHAKO, SHETANI AKISHINDWA KUKIZUIA, ATAKITUMIA KAMA MTAJI WAKE KUKULETEA KIBURI.

Shetani akishindwa kukuzuia jambo zuri, atalitumia kinyume nawe na kinyume na Mungu wako.

Akishindwa kukuzuia kupata kazi atataka atumie hiyo kazi kukupatia kiburi, akishindwa kuzuia afya atataka akupatie kiburi cha kuwa na afya... Uone wasio na afya hawana Mungu au wamemkosea Mungu.

Anatumia KIZURI kukufanya ujione bora kuliko wengine, ujilinganishe na wengine, ujione ni wa pekee, na wengine wako chini.

KIBURI hukufumba macho usione mchango na umuhimu wa watu wengine wakati huohuo hukufumbua macho ya kiburi UJIONE ZAIDI YA ULIVYO.

Mungu akikupa kitu kizuri hakusudii KUKUFANYA UJIONE NI BORA KULIKO WENGINE, BALI NI ILI UWE TAYARI KUKITUMIA PAMOJA NA WENGINE AMBAO NAO WAKO BORA KWENYE ENEO LINGINE [AMBALO WEWE SI BORA] ILI KUJENGA KWA PAMOJA.

Ubora anaotupatia Mungu ni kwa ajili ya kuwafaa wengine na kushirikiana na si kutufanya sisi wakipekee na bora kuliko wengine au kuwadharau wengine.

Lengo la Mungu kukubariki ni ili uwabariki wengine na sio kukuza kiburi chako. Lakini Shetani anataka atumie baraka aliyotubariki Mungu kutukosanisha na Mungu wetu kwa kuinua Kiburi.

KWA UPANDE WA PILI, dhambi hii ya KIBURI, itaikuza AIBU YA KOSA KULIKO UHALISIA WAKE.

Yaani, Mtu akikosea, dhambi hii ndani yake itamfanya AONE KWAMBA, AKIKUBALI KOSA ATAAIBIKA. AKIKUBALI KOSA ATAONEKANA MNYONGE, AU ALIYESHINDWA.

Ukweli ni kwamba, KUKUBALI KOSA NA KUTUBU AU KUOMBA MSAMAHA NI ISHARA YA USHINDI NA UNYENYEKEVU.

Kushindwa kuomba msamaha au kukubali kosa HUONYESHA KIBURI CHA MTU KIKO KAZINI.

KIBURI NA AIBU HUAMBATANA ndio maana Neno la Mungu linasema katika kitabu cha Mithali 11:2 Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.

Kwa lugha rahisi ni kwamba, DHAMBI YA KIBURI HUKUONYESHA HESHIMA AMBAYO HUNA, lakini pia, HUKUONYESHA AIBU AMBAYO HAIPO.

HUIKUZA HESHIMA YA MTU MACHONI PAKE MWENYEWE,       NA PIA HUIKUZA AIBU YA MTU MACHONI PAKE MWENYEWE, LAKINI KWA UHALISIA WAKE HAKUNA HESHIMA YA KIWANGO HICHO WALA HAKUNA AIBU YA KIWANGO HICHO AU INAWEZEKANA HAKUNA HESHIMA KABISA AU HAKUNA AIBU KABISA.

Kiburi kinatusahaulisha UHALISIA WA MAISHA, kinatusahaulisha KIFO,     kinatusahaulisha kwamba KILA KIZURI AMETUPA MUNGU NA YEYE NDIYE ANAWEZA YOTE, kinatusahaulisha kwamba TUMEPEWA KWA AJILI YA WENGINE NA SIO KWA AJILI YETU TU, kinatusahaulisha HAPA DUNIANI HAKUNA KINACHODUMU vyote vinapita.

Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.

MIT. 16:18

Kwa hiyo, MAADAM TUNAISHI DUNIANI, Ni lazima TUFANYE MAAMUZI KILA SIKU, KUISHINDA DHAMBI HII YA KIBURI.

"KIBURI HUTANIHARIBU KWA JINA LA YESU"

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula

 

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!