Hatia Haitoki Kwa Mungu
Matendo ya Mitume 22:7-10 SUV
"Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye."
Sauli alipokutana na Yesu alikuwa ni muuaji na mtesaji wa kanisa, na kwa ukweli alikuwa akimuudhi sana Yesu!
Lakini ninashangaa Yesu alipomwambia tu anamuudhi aliishia hapo!
Yesu angeweza kuanza kumlaumu kwa kuendelea kuzungumzia ukubwa wa makosa yake na madhara aliyosababisha kwa kanisa na kumfanya Sauli asikie hatia zaidi na kujilaumu sana kwa makosa yake!
Lakini badala yake, hakuendelea kumlaumu bali alimwambia cha kufanya.
Nafikiri na sisi tuna kitu cha kujifunza sana hapo, mara nyingi tunapokosewa, tunatumia muda mwingi sana kuwalaumu waliotukosea na kujaribu kuwaonyesha ukubwa wa makosa yao kwa lengo la kuwafanya wasikie hatia sana ndani yao, na wakati mwingine tunaendelea kuwasema na kuwasimanga hata kama wameshaonyesha kwamba wamegundua makosa yao.
Kwa kweli tunapofanya hivyo TUNAMSAIDIA SHETANI KAZI na wala si Mungu...
Neno la Mungu linasema katika
Wakolosai 3:13 "mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi."
Kwa hiyo, hata kama tunayo sababu na ni kweli tumekosewa, tuwe makini kwenye eneo hilo.
Ukifuatilia maandiko utagundua kuwa Shetani ndio huleta hatia na kujilaumu au hututaka tulaumu maana yeye ni MSHITAKI wetu.
Roho Mtakatifu akikuonyesha kosa au dhambi haishii hapo na kuanza kukulaumu, bali hukujulisha cha kufanya!
Unapokataa kufuata maelekezo ya Neno la Mungu kuhusu dhambi hapo ndipo unafungua mlango wa Shetani kukushitaki na kuachilia HATIA ndani yako.
Ukikimbilia kwa YESU, Yesu atakusamehe dhambi na kukuambia "usitende dhambi tena".
"Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena." Yohana 8:10-11 SUV
KUMBUKA HUYU MAMA ALIKAMATWA AKIFANYA UZINZI, lakini Yesu hakumuhukumu alipokimbilia kwake.
Unapokosea, ukikimbilia kwa Yesu, hata siku moja Yesu hakuhukumu; Ukiona umekimbilia kwa Yesu na bado una hali ya hatia na hukumu, uwe na uhakika hali hiyo haitoki kwa Mungu.
Hukumu au Hatia hiyo yaweza kuja kwa ADUI KUKUHUKUMU, AU WEWE MWENYEWE KUJIHUKUMU, zote sio sahihi.
Sasa hii haimaanishi tucheze na dhambi hapana, atendaye dhambi makusudi kwasababu tu Mungu husamehe, huyo ni mpumbavu na hajui maana ya Neema na kimsingi anamfungulia shetani mlango na shetani anaweza kumnyonga kama alivyofanya kwa Yuda aliyemsaliti Yesu.
Ninachotaka uone ni kwamba, Sauti ya Mungu ikikujulisha kosa au dhambi hukuambia cha kufanya, sauti ya Shetani ikikujulisha kosa hukuletea mashitaka, hatia na kujilaumu tu ndani yako.
Roho Mtakatifu alimjulisha Petro cha kufanya baada ya dhambi ya kumkana Yesu mara tatu, na Yesu alimsamehe kabisa.
Kama umekosea au ukikosea, Piga hatua, usikae kujilaumu amua cha kufanya sawa na Neno la Mungu.
Shetani anataka ukijikwaa na kuanguka ukae hapohapo chini, Neno linasema Mwenye haki akianguka huinuka tena.
Usikubali kuendelea kukaa kweye anguko la dhambi; inuka, tubu na uache kabisa.
Angalizo: Kama kila mara dhambi hiyo hiyo hukuangusha, maana yake ni kwamba, kuna nguvu nyuma ya dhambi hiyo ambayo inakutawala ndani yako, kwa hiyo toba binafsi pekee haitakufungua, unahitaji msaada zaidi wa Kiroho toka kwa mtumishi wa Mungu mwaminifu!
Kumbuka pia: Kila anayeizoelea dhambi, hufungua mlango kwa pepo linaloitawala dhambi hiyo kumuingia, na ikifika point hiyo toba binafsi itaachilia tu msamaha, lakini haiwezi kuondoa hilo pepo; ndio maana unakuta mtu kila siku anatubu na kuanguka kwenye dhambi hiyo hiyo... usife kiume, tafuta msaada wa kiroho ufunguliwe!
Lakini pia, kuna watu ambao, kwa sababu moja au nyingine wameshafungulia mlango wa HATIA TOKA KWA SHETANI, na ijapokuwa wameshatubu mara nyingi, bado roho ya HATIA inawatesa! Binafsi nimekutana na watu wa aina hiyo. Kama uko kwenye hatua hiyo, tafuta msaada wa Mtumishi wa Mungu haraka sana kwa sababu lengo la shetani sio kukuletea hatia tu bali ni kukufikisha alipomfikisha Yuda... akamuua!
Shetani alimletea Yuda hatia mpaka Yuda akajiua.
Mithali 28:13 SUV "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema."
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author