Hauruhusiwi Kuwa Masikini
Kumbukumbu la Torati 15:4-5 SUV
"Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;) kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya."
Kama Mungu aliwaapia Israel kwamba kama wataisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, HAWATAKUWAKO MASIKINI KWAO; vipi kwetu sisi tuliookoka?
Neno la Mungu linasema, Sisi tunaishi katika agano lililobora zaidi ya waliloishi Israel.
"basi kwa kadiri hii Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi." Waebrania 7:22
"Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora." Waebrania 8:6
Maana yake kwetu sisi ni marufuku kuwa masikini!
Ukifuatilia maandiko, utagundua umasikini ulikuwa ni moja ya AJENDA ZA YESU alizozishughulikia alipokuja duniani!
Labda tuanzie kwenye kuelewa kwanza umasikini ni kitu gani...
Maana kuna watu wanafikiri umasikini ni kutokuwa na pesa, hapana, kutokuwa na pesa au mali inaweza kuwa ni matokeo tu lakini sio tafsiri sahihi ya umasikini.
Yesu alisema nini kuhusu masikini au umasikini?
Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema...LK. 4:18a SUV
Umasikini ni nini sasa?
Umasikini ni kutokuwa na habari njema.
Umasikini ni kutokuwa na taarifa sahihi zinazoweza kukukwamua toka ulipokwama.
Umasikini ni kutojua cha kufanya unapokutana na changamoto ya kimaisha au kifedha.
Kwa hiyo, kama sina pesa au mali kwa sasa lakini nina habari njema yaani ninajua cha kufanya, nina taarifa sahihi, ili nitoke nilipo hatua kwa hatua mpaka nifikie mahali fulani (hata kama itachukua muda mrefu), mimi si masikini.
Sasa turudi kwenye andiko letu la msingi:-
"Lakini hawatakuwako maskini kwenu; (kwa kuwa BWANA atakubarikia kweli katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki, iwe urithi wako;) kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya." Kumbukumbu la Torati 15:4-5 SUV
Mstari wa tano Mungu amesema HAWATAKUWAKO MASIKINI, lakini msitari unaofuata ameweka masharti akisema, "kwamba utaisikiza tu kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, uyatunze maagizo haya yote nikuagizayo leo, kuyafanya."
Kwa hiyo, kila atakayeisikiza kwa bidii sauti ya Bwana (HABARI NJEMA), hawezi kuwa masikini kamwe!
Tunasikiza sauti ya Mungu kwa kulisoma Neno lake.
Tunasikiza sauti ya Mungu kwa kumsiliza Roho Mtakatifu.
Tunasikiliza sauti ya Mungu kwa kusikiliza mafundisho sahihi.
Maana yake ni nini?
Maana yake ni kwamba, kwenye kila hali unayopitia, hata kama inaweza kuonekana ni ya umasikini, hauruhusiwi kukaa hapo; MUNGU ANAYO MAELEKEZO ya kukutoa hapo.
Sauti ya Mungu inayo maelekezo ya nini cha kufanya ili kukufanya usiwe masikini.
Inayo maelekezo ya kibiashara, inayo mawazo ya kibiashara na ya kimaisha yanayoweza kukukwamua kutoka kwenye kila hali.
Tatizo letu tunamuwekea Roho Mtakatifu mipaka, kwamba atusaidie tu kuomba na kusoma Neno na mambo mengine ambayo tunayaita ni ya Kiroho, TUNASAHAU HATA KUTOKA KATIKA UMASIKINI NA HALI NGUMU NI JAMBO LA KIROHO, tukimruhusu atatushauri MRADI WA KUFANYA, NAMNA YA KUUFANYA ili kututoa.
Lakini pia anachomaanisha Mungu ni kwamba, kwenye Neno la Mungu ziko kanuni za Ki-Mungu au za ufalme wa Mungu zinazoweza kumfanikisha mtu na kumtoa kwenye umasikini kwa njia halali kabisa bila kumkosea Mungu.
Tuanze kumruhusu Mungu atuonyeshe namna ya kutoka katika hali ngumu.
Tuanze kumruhusu Roho Mtakatifu kutupatia mawazo ya Kibiashara na kikazi na miradi ya kufanya tuone kama hatatushauri jinsi ya kujikwamua.
Tuanze kulisoma Neno la Mungu na kusikiliza mafundisho sahihi kwa lengo la kupata kanuni za UFALME WA MUNGU za kutoka kwenye hali ngumu za maisha, na tukizipata kanuni hizo tuzifanyie kazi, na kuhakikishia NENO LA MUNGU NI KWELI KABISA "HATUWEZI KUWA MASIKINI"
Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake. 2 Wakorintho 8:9 SUV
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author