Text

Kaa Katika Neno la Mungu

1 views 1 day ago

Yohana 8:31b-32

“Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.”

NKJV: Then said Jesus to those Jews which believed on him, If ye continue in my word,

Yohana 15:7 “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.”

Kaa katika Neno la Mungu!

Kukaa katika Neno ni kuamua kuliamini Neno la Mungu, ni ku settle kwenye Neno la Mungu ni kuamua kutulia (ku-rest) kwenye Neno la Mungu.

Ukifuatilia maana ya Neno hili kukaa ni sawa na KUGUNDUA ENEO FULANI NA KUKAA HAPO, lugha nyingine iliyotumika ni KUSUBIRI MAHALI KWA UVUMILIVU BILA KUONDOKA, au KUENDELEA KUKAA BILA KUCHOKA.

Ni Kukaa kwenye eneo fulani, hali fulani au matarajio fulani BILA KUONDOKA HAPO, huko ndio kukaa kulikozungumziwa hapa.

Yesu Anasema, TUKIKAA KWENYE NENO LAKE, yaani tukiamua ku settle hapo kwenye kile Neno la Mungu linasema bila kuyumbishwa wala kubadilishwa na MAZINGIRA YANAYOENDELEA NJE, tukifanya hivyo mambo matatu yatatutokea

1) Tumekuwa wanafunzi wake kweli kweli

2) Tutaijua kweli ambayo itatuweka huru

3) Tutatendewa kila tutakachoomba (sawa na Neno)

Mtu wa Mungu, nakutia moyo, endelea kukaa katika Neno la Mungu, endelea KULIAMINI NENO LA MUNGU! Hata kama hujaona matokeo ENDELEA... Weka MIZIZI KATIKA NENO, JICHIMBIE HUMO KWENYE NENO, USIYUMBISHWE NA UNAYOYAONA, YOTE UNAYOYAONA YANAWEZA KUBADILISHWA NA NENO LA MUNGU.

Giza linaweza kugeuzwa na Neno, kwa hiyo giza lisikusababishe utoke kwenye Neno, Ukiwa, utupu vyote vinaweza kugeuzwa na Neno la Mungu, kaa kwenye Neno.

Vyote vilifanyika kwa NENO, kwa hiyo hata visivyokuwepo vinaweza kufanyika kwa Neno, kwa hiyo kaa KWENYE Neno.

Afya isiyokuwepo INAWEZA KULETWA NA NENO, AMUA KUKAA KWENYE NENO.

Uadilifu wa Neno la Mungu haupimwi na Mazingira, UADILIFU WA NENO NI UADILIFU WA MUNGU, kwa hiyo Mungu ndiye anausimamia.

Neno la Mungu lazima litatimiza makusudi yake kwenye maisha ya MTU AMBAYE AMEAMUA KULIAMINI BILA KUJALI MAZINGIRA YANAYOMZUNGUKA.

Isaya 55:11 “ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

HAIWEZEKANI ULIAMINI NENO NA UAMUE KUKAA KWENYE NENO HALAFU LISIZALISHE MATOKEO, HAIWEZEKANI.

Tatizo letu ni kuwa na MACHAGUO (ALTERNATIVES), kwamba, ninajaribu Neno la Mungu nikishindwa nitajaribu kitu kingine.

Ukiamua KULIAMINI NENO LA MUNGU, USIFANYE KWA MAJARIBIO, AMUA KULIAMINI HILO PEKEE KWA SABABU NDILO PEKEE LISILOSHINDWA.

Neno linasema, katika Zaburi 1:2-3 “Bali sheria ya BWANA ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. [3] Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.”

Mtu aliyeamua KUKAA KWENYE NENO (ku-settle, kulifanya Neno la Mungu ndio tamko lake la mwisho), atakuwa kama mti uliopandwa kandokando ya vijito vya maji, Atazaa matunda kwa majira yake, Hatanyauka, na Kila alifanyalo litafanikiwa.

Neno la Mungu limebeba MAFANIKIO YETU. AMUA KUKAA KWENYE NENO.

HAYA SIO MAAMUZI YA KIMATUKIO, yaani KUKAA KWENYE NENO SIO TUKIO BALI NI MAISHA...

NI UAMUZI WA MAISHA SIO TUKIO LA MUDA MFUPI.

Sio jambo la kusema, mwezi huu wote nakaa kwenye Neno nione nini kitatokea.

Kukaa kwenye Neno ni kuamua kwamba, MAISHA YANGU YOTE NINAAMUA KUJIFUNZA NENO LA MUNGU KWA BIDII ZOTE NA KULIFANYA NENO LA MUNGU KUWA NDIO SAUTI YA MWISHO YA MAISHA YANGU, SITAKUBALI MAZINGIRA YANIHUBIRIE TENA, NITASHIKA KILE AMBACHO NENO LINASEMA TU. KILA KINACHOTOKEA NITAKIPIMA NA NENO LA MUNGU, KAMA KINAENDANA NA NENO NITAKIKUBALI KAMA KINAPINGANA NA NENO SITAKIPOKEA.

Mungu anamuhimiza Yoshua katika Yoshua 1:8 “Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.”

Kwamba MAFANIKIO YAKO YAMEWEKWA KWENYE NENO LA MUNGU, lisiondoke Neno Kinywani mwako, litafakari (lifikiri, liwaze, lifanye kiongozi wako) mchana na usiku, NDIPO UTAFANIKIWA NA KUSITAWI.

Lazima tufanye maamuzi ya KUKAA NDANI YA NENO.

Andiko tulilonukuu linasema "Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa"

Anaposema mkikaa "ndani yangu" kimsingi anasema "Ndani ya Neno" sababu Yesu ni Neno.

Kwa hiyo Sisi tunakaa ndani ya Neno, tunafunikwa na Neno, na hilo Neno linakaa ndani Yetu, yaani TUNACHANGANYIKANA.

Unajilisha (Unakula) Neno kiasi kwamba mpaka Neno linakumeza wewe. Linameza mawazo yako, Unawaza sawa sawa na Neno, linameza maneno yako, UNASEMA SAWA SAWA NA NENO, linameza maisha yako, UNAISHI NA KUYATAZAMA MAISHA SAWA SAWA NA NENO.

Ezekieli 3:1-3 “Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.”

Dhamiria tangu sasa KUKAA KATIKA NENO, DHAMIRIA KUJILISHA NENO KILA SIKU, KILA WAKATI NA UTAONA MATOKEO YAKE.

Usikubali kutafakari mawazo au taarifa ZINAZOPINGANA NA NENO LA MUNGU hakikisha kila unachoruhusu kukiwaza kinaendana na Neno.

HAKIKISHA UNAFIKIRI SAWA NA NENO, UNAOMBA SAWA NA NENO NA UNATAMKA SAWA NA NENO.

FANYA MAAMUZI LEO, KAA KATIKA NENO LA MUNGU, UTAANZA KUONA UNAKUWA MWANAFUNZI MZURI WA YESU LAKINI PIA UTAONA MUNGU AKIJIBU MAOMBI YAKO KWA HARAKA.

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

Umebarikiwa

~Na. Mwl. Francis M. Langula

(+255754711247)

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!