Kama Haimfai Yesu (Ufalme wa Mungu) Itanyauka
Marko 11 13-14 “Akaona kwa mbali mtini wenye majani, akaenda ili labda aone kitu juu yake; na alipoufikilia hakuona kitu ila majani; maana si wakati wa tini. Akajibu, akauambia, Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako. Wanafunzi wake wakasikia.”
Kuna jambo hapa nimeliona napenda tuliangalie pamoja.
Huu mtini ulikuwa umestawi na kunawiri, na Yesu alitegemea angepata matunda lakini hakupata matunda sababu haukuwa wakati wa tini.
Baada Yesu kukosa matunda ndipo akauambia Mtini "Tangu leo hata milele mtu asile matunda kwako."
Kwenye haya maneno kuna kanuni naiona.
Kama Unachokifanya au ninachokifanya hakimpatii Yesu matunda, kinapoteza uhalali wa kuzaa matunda.
Hata kama mtini umestawi kiasi gani, maadam Yesu akija hawezi kula matunda, basi ule mtini hauna uhalali wa kuendelea kuzalisha matunda.
Salama ya mtini ilikuwa kuzalisha matunda kwa ajili ya Yesu kwanza, ndipo ungeweza kuendelea kuzalisha kwa wengine.
Si kwamba Yesu alikuwa anakuja kula matunda kwa mtini kila siku, lakini ilikuwa ni muhimu sana siku anayotaka matunda ayapate.
Uhakika wa Ustawi wetu na kuzaa matunda kwetu ya kutufaa na kuwafaa wengine una muunganiko na Yesu kula kwanza matunda yetu.
Kama Yesu akila matunda ya kile ninachokifanya, ninachokifanya kitaendelea kuzaa matunda ya kunifaa mimi na wengine, vinginevyo kuna uwezekano wa kunyauka.
Nafananisha ujumbe wa andiko hili na ujumbe wa KUUTANGULIZA UFALME WA MUNGU KAANZA.
Kila tunachokifanya, KIMFAE YESU KWANZA NA UFALME WAKE.
Lazima tutambue kwamba SISI NI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU (WE ARE FOR THE KINGDOM), MAFANIKIO YETU NI KWA AJILI YA UFALME WA MUNGU, KUTOJITOA NA KUTOTOA KWA AJILI YA UFALME KUNAWEZA KABISA KUNYAUSHA TUNACHOKIFANYA.
Kama UJANA WAKO haumfai Yesu hautamfaa mtu.
Kama biashara yako haimfai Yesu (Ufalme wa Mungu) haitamfaa mtu mwingine
Kama chombo chako hakimfai Yesu, hakitamfaa mtu mwingine
"Kwa Neno lako nitazishusha nyavu"
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa
~Na Mwl. Francis M. Langula
+255754711247
Mwl. Francis Langula
Author