Kama Ilivyo Tanuru Kwa Dhahabu Ndivyo Alivyo Mungu Kwa Mioyo Yetu.
Mithali 17:3
“Kalibuni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Bali BWANA huijaribu mioyo.”
Kalibuni hutumika kwa ajili ya kung'arisha na/au kuyeyusha madini fedha (silver), na TANURU ni kwa ajili ya kuyeyusha na kung'arisha dhahabu. Ung'arishaji na uyeyushaji huu ni kwa kutumia moto mkali maalum, kwa hiyo ukiona madini fedha(silver) au dhahabu yanang'aa, ujue yamepita kwenye moto mkali maalum, Kalibuni au Tanuruni.
Kwa hiyo kazi ya tanuru ni kung'arisha Dhahabu na kazi ya Kalibu ni kung'arisha madini fedha, lakini kinachonishangaza zaidi kwenye maandiko haya ni jambo la tatu baada ya Kalibu na Tanuru. Mungu anasema, kama Kalibuni na Tanuru zilivyo na kazi kwa madini fedha na dhahabu, NDIVYO ALIVYO MUNGU KWA MOYO WA MWANADAMU.
Kwa mifano iliyotangulia ni wazi kwamba Mungu hutumia mbinu zile zile za Kalibuni na Tanuru kwa dhahabu na fedha kwa mioyo yetu.
Kwa kadiri Moto wa Tanuru unavyokuwa mkali ndio kwa kadiri hiyo hiyo dhahabu huwa bora au hung'aa. Moto mkali sana ni kwa dhahabu bora sana.
Kweli hii ni nzuri sana na rahisi kuielezea KWENYE DHAHABU, lakini kwenye MIOYO YETU, jambo hili ni gumu sana kulielewa.
Ni rahisi sana KUUELEWA MOTO LINAPOKUJA SWALA LA KUING'ARISHA DHABIHU AU KUIFANYA DHAHABU KUWA BORA, lakini SIO RAHISI SANA KUUELEWA MCHAKATO WA MAJARIBU NA MATESO LINAPOKUJA SWALA LA MIOYO YETU.
Nikama vile KUNA NJIA MBADALA YA KUTUNG'ARISHA BILA KUPITIA MCHAKATO WA MOTO.
Lakini Neno la Mungu limeweka wazi kabisa kwamba, KAMA VILE KALIBUNI KWA FEDHA NA TANURU KWA DHAHABU NDIVYO ALIVYO BWANA KWA MIOYO YETU.
Kinachonifurahisha hapa ni namna ambavyo MUNGU ANATHAMINI MIOYO YETU, AMEONA YEYE NDIYE AIPIME NA MOTO WAKE.
“Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.” Isaya 43:2
Sio kila maji mengi na mito hugharikisha...
Kazi ya moto sio tu kuteketeza, MOTO MWINGINE HUONGEZA MNG'AO WA DHAHABU PIA.
Tatizo la mchakato wa moto ni kwamba NI NGUMU SANA KUUELEWA MCHAKATO WENYEWE HASA WAKATI UNATUKIA, NI RAHISI SANA KUDHANI KWAMBA UNATEKETEA AU UNATESWA lakini ukweli ni kwamba HAUTEKETEI BALI UNANG'AA.
Kuna MNG'AO fulani HATUWEZI KUUPATA MAHALI PENGINE POPOTE ISIPOKUWA KWENYE MAJARIBU
“Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.” 1 Petro 1:6-7
“Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.” Yakobo 1:2-3
“Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.” Ayubu 23:10
Mwamini aliyeruhusu moyo wako ujaribiwe, uamini MCHAKATO WENYEWE kwa sababu kama VILE TANURU ILIVYO NA UZOEFU LINAPOKUJA SWALA LA KUING'ARISHA DHAHABU NDIVYO ALIVYO MUNGU KATIKA KUIJARIBU MIOYO NA KUITOA KAMA DHAHABU.
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author