KUNA KUINUKA TENA
AYUBU 22:29 “Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.”
Unahisi kuna mtu amekuangusha? au Amekuwa sababu ya kurudi kwako nyuma kimaisha, kiroho, kibiashara kikazi nk?
Ulikuwa na bidii na mambo ya Mungu lakini kuna mtu ni kama amekurudisha nyuma, amekuangusha?
Ulikuwa una mafanikio lakini ghafla ni kama kuna mtu amekutia hasara? Au Ulimpatia mtu pesa amekudhul umu na ukiangalia ni kama amekurudisha nyuma au kukuangusha kabisa?
Huyo mtu unaweza kuwa ni wewe mwenyewe, umefanya makosa fulani na ukagundua umeanguka, yaweza kuwa kiroho au kimaisha au kibiashara au eneo lolote la maisha!
Inawezekana hakuna aliyekuangusha wala wewe mwenyewe hauhusiki moja kwa moja, ni hali tu imebadilika na ukajikuta UMEANGUKA, MTAJI UMEKATA, KAZI ULIYOTEGEMEA IMEISHA, MAHALI ULIPOWEKEZA PAMEKUFA, AFYA IMEANGUKA NK....
Neno la Mungu linakujia leo kukuambia, KUNA KUINUKA TENA!
MIKA 7:8 “Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu.”
Ukigundua umeanguka katika eneo lolote la maisha, kwa sababu yoyote ile, DAWA YAKE SIO KUJILAUMU au kulaumu watu bali DAWA YAKE NI KUINUKA TENA!
Hata kama unaona hakuna dalili za kuinuka, usiho fu, maadam Yesu ni Bwana kwako, UTAINUKA tu, YESU atakuwa NURU kwako!
Ndio maana Neno linasema “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.” AYUBU 19:25
NENO PIA LINASEMA "Kwa maana mwenye haki huanguka mara saba akaondoka tena; Bali wasio haki hukwazwa na mabaya." MITHALI 24:16
Mwenye haki akianguka huinuka haraka
Hata kama umejaribu kuinuka na ukaanguka tena, haimaanishi kwamba hautainuka tena!
Usije ukaniona nimeanguka ukadhani nitakaa hapo hapo!
Usije ukaniona nimekatwa ukadhani sitachipuka tena!
Usije ukajiona umeachishwa kazi ukafikiri hautaweza Kuishi tena, Mungu hana chanzo kimoja! Mungu ni Mungu wa NJIA NYINGI [MTENGENEZA NJIA] NI MUNGU WA MILANGO MINGI
Usije ukajiona umefil isika ukadhani hutainuka tena, MUNGU anaweza KUMTOA MYONGE JAANI NA KUMKETISHA PAMOJA NA WAKUU! Zaburi 113:7-8
Usije ukajiona afya yako imeporomoka na madaktari wanasema hii case yako imeshindikana ukadhani utakufa na huo ugonjwa
NENO LA MUNGU LINASEMA:-
Kwani yako matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena, Wala machipukizi yake hayatakoma. Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, Na shina lake kufa katika udongo; Lakini kwa harufu ya maji utachipuka, Na kutoa matawi kama mche.
AYU. 14:7-9 SUV
Usikate tamaa, utachipuka tena..., usiogope utainuka tena, kiafya, kibiashara, kifedha, kihuduma, kiroho!
Maadam nia ipo, na uko mahali sahihi kwa YESU KRISTO ambaye ndiye chanzo cha kila kitu, usijali unachoona kinatokea, LAZIMA UTACHIPUKA TENA, LAZIMA UTASTAWI TENA!
Jambo la Muhimu, USIONDOKE KWENYE CHANZO ambaye ni YESU!
Ni watoto tu ndio wakianguka wanalala hapohapo ili wainuliwe na kuonewa huruma, mtu mzima akianguka anainuka mara moja na anaangalia alijikwaa wapi au nini kilimuangusha ili kujifunza na anasonga mbele kwa tahadhari!
Usikate tamaa, KUNA KUINUKA TENA! UTAINUKA TENA
Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa. AYUBU 22:29
Hata kama mpaka sasa unajiona bado uko chini, KUNA KUINUKA TENA! FANYA MAAMUZI SAHIHI, INUKA TENA...
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
Mwl. Francis Langula
Author