Kwenye Uwepo wa Mungu(Maombi) ni Mahali Pa Kuongezewa Nguvu Kukabiliana na Changamoto
Mathayo 26:38
“Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”
Luka. 22:41-44
“Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. [Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]”
Yesu alipokaribia kwenda msalabani, ilifika mahali mwili ulikuwa hautaki na huzuni ilimfunika kubwa mno.
Tafsiri nyingine ya Biblia inasema, "Moyo wangu umelemewa na huzuni, kiasi kwamba najisikia hali ya kufa"
Kwa hiyo Yesu alifika mahali akawa amezidiwa na huzuni kwa kile kilicho mbele yake au kinachomkabili;
Nina uhakika kila mtu anaweza akawa amewahi kuwa na hali hiyo, hali ya huzuni na kukata tamaa kwa sababu ya yale yanayomkabili, Kujihisi kama kufa kufa, kujihisi huna nguvu tena za kuendelea!
Wengine wanaposoma ujumbe huu, kuna changamoto wanazipitia zimewafikisha kuhisi ninachokielezea, kuhisi kukata tamaa, kuhisi kama kufa ndio kuko mbele yao, a idha kufa kwa miili yao au kufa kwa matarajio yao au hatma zao au hata kujiua!
Kusudi la Tafakari hii ni KUJIFUNZA YESU ALIFANYA NINI KILICHOMSAIDIA KATIKA HALI HIYO?
Neno la Mungu linasema: “Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.” Mathayo 26:38
Yesu alipogundua amezidiwa na hali hiyo, alitafuta watu(Petro, Yakobo na Yohana) aliowaamini kwamba wanaweza kumsaidia kuubeba huo mzigo(ingawa hawakuweza kumsaidia kuubeba) kisha AKAKIMBILIA KWENYE UWEPO WA MUNGU(KWENYE MAOMBI)!
Na hapo ndipo tunapopishana, wengine wakipatwa na hali ya kukata tamaa na huzuni iliyopitiliza hukimbilia kulala, au kuwaeleza watu wasio sahihi au kunung'unika au kufanya kitu kingine chochote lakini sio kwenda uweponi mwa Mungu(KUOMBA)...
Lakini wengine wanakimbilia katika maombi ila si kuomba bali ni kulalamika na kunung'unika kwa hiyo hawapati msaada unaohitajika!
YESU ALIKAA KWENYE MAOMBI au KWENYE UWEPO WA MUNGU MPAKA ile hali ya huzuni kiasi cha kufa ilimuachia, na akawa tayari sasa kukabiliana na kile kilichokuwa mbele yake!
Kwenye andiko tulilonukuu u, tunaona Yesu alikaa kwenye uwepo wa Mungu mpaka malaika alikuja kumtia nguvu.
Kazi ya maombi au uwepo wa Mungu sio tu kuliondoa tatizo, bali pia ni KUTUTIA NGUVU KUKABILIANA NA CHANGAMOTO HUSIKA MPAKA USHINDI!
Unapokutana na changamoto na unasikia hali ya kushindwa na kukata tamaa, KIMBILIA UWEPONI MWA MUNGU KWA NJIA YA MAOMBI NA USITOKE HUKO MPAKA UMETIWA NGUVU!
KWENYE UWEPO WA MUNGU NDIPO ZILIPO NGUVU ZETU KUKABILIANA NA CHANGAMOTO MBALI MBALI ZA MAISHA!
Ukikutana na majaribu au changamoto zinazokushinda, usikimbilie kujifungia chumbani kulia na kunung'unika; bali KIMBILIA UWEPONI MWA MUNGU, MAANA UWEPONI MWA MUNGU ZIKO NGUVU, NI MAHALI TUNAPOTIWA NGUVU!
“Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake. Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.”
EBR. 2:17-18 SUV
Yesu anafuzu kuwa K uhani M kuu wetu kwa sababu alipitia tunayoyapitia, alijaribiwa kama tunavyojaribiwa hata zaidi, kwa hiyo ANAWEZA KABISA KUTUSAIDIA TUNAPOJARIBIWA!
“Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo.
bali wao wamngojeao BWANA watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”
ISA. 40:29, 31 SUV
Usikubali HUZUNI NA KUKATA TAMAA VIKAKUMEZA, KIMBILIA KWENYE UWEPO WA MUNGU, NA USITOKE HUKO MPAKA UMETIWA NGUVU, MNGOJE BWANA HUKO MPAKA UMEPATA NGUVU MPYA!
-- Wapo malaika wanakusibiri uweponi mwa Mungu ili wakutie nguvu kama walivyofanya kwa Yesu! Nenda uweponi mwa Mungu ukapokee msaada wako kuendelea mbele!
-- At God's presence is the place for our strength!
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
Mwl. Francis Langula
Author