Text

Lakini yako Inamuhitaji Mtu

1 views 1 day ago

2 Wafalme 5:1Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake BWANA alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma.
2 Kings 5:1 AMP Now Naaman, commander of the army of the king of Aram (Syria), was considered a great man by his king, and was highly respected because through Naaman the Lord had given victory to Aram (Syria). He was also a man of courage, but he was a leper.
Neno la Mungu nililonukuu hapo juu, limeweka wazi kwamba, Naamani alikuwa mtu mkuu katika nchi ya Shamu. 
Alikuwa Jemadari wa Jeshi au kwa lugha ya sasa ni Mkuu wa Majeshi wa Shamu. 
Mfalme wa Shamu alikuwa anamuhesabu kama mtu mkuu  sana (considered a great man by his king).
Alipewa Heshima kubwa au ya juu sana kwa sababu kupitia yeye, Mungu aliwapa ushindi Shamu kwenye vita vyao. 
Alikuwa Mtu hodari sana wa vita, yaani mwenye nguvu, umahiri na uweledi katika maswala ya vita. 
Pamoja sifa hizo zote, LAKINI ALIKUWA NA UKOMA. 
UKOMA ni ugonjwa unaokula ngozi na ambao haukuwa na tiba, lakini pia ulikuwa ni kati ya MAGONJWA NAJISI kipindi kile. Yaani, Kwa Israeli, mtu mwenye ukoma alikuwa anatengwa kabisa na jamii. 
Sasa Naamani, Pamoja na nafasi nzuri aliyokuwa nayo, na heshima zote alizokuwa nazo LAKINI ALIKUWA NA UKOMA. 
Alikuwa na tatizo kubwa linalomsumbua. Ukoma ulikuwa ni ugonjwa usio na tiba; Ninaamini kwa nafasi na uwezo wake hata kama tiba yake ingegharimu kiasi chochote cha pesa angemudu. 
2 Wafalme 5:13 Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?
Kupona UKOMA ilihitaji MUUJIZA TU na sio vinginevyo. 
UKOMA ulikuwa ni "LAKINI" ya Naamani.
Alikuwa Jemedari wa jeshi LAKINI alikuwa na UKOMA.
Alikuwa Mtu mkubwa Mbele ya Mfalme LAKINI alikuwa na UKOMA.
Alikuwa na Heshima kubwa sana katika nchi LAKINI alikuwa na UKOMA.
Alifanikishwa sana kwa Mkono wa Mungu juu ya maisha yake, LAKINI alikuwa na UKOMA.
2 Wafalme 5:2-3 Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.
"LAKINI" ya Naamani ilimuhitaji MTU aliyetumwa na Mungu ili amuonyeshe Naamani MTUMISHI WA MUNGU wa Kweli anayeweza kumsaidia na kumvusha hapo. 
Mungu akamletea mjakazi, mfungwa, kwenye nyumba yake ili amtumie kumuelekeza alipo NABII WA MUNGU.
Jambo lingine ni kwamba, "LAKINI" ya Naamani, ilimtaka Naamani akubali kuweka pembeni cheo chake, heshima yake na akubali kwamba ANALO TATIZO, na kwamba MAFANIKIO YAKE YOTE HAYAWEZI KUMSAIDIA TATIZO la UKOMA KATIKA MWILI WAKE. 
Ashukuriwe Mungu kwa sababu Naamani hakukubali "Kufa kiume na tai shingoni", aliamua kuweka heshima yake chini na kuamua mwenda kwa Mtumishi wa Mungu kutaka msaada.
Kuna watu wengi sana wanazo "LAKINI" na wamezificha kwenye Mafanikio yao.
Ni kweli wewe ni muimbaji mzuri sana LAKINI tamaa mbaya inakutesa.
Ni kweli kwenye eneo la Pesa au biashara uko vizuri LAKINI UZINZI UMEKUSHINDA.
Ni kweli ni KIONGOZI KANISANI, Unahubiri kabisa, au UNAYO DINI NZURI, KANISA ZURI LAKINI DHAMBI IMEKUSHINDA... Dhambi inakutesa.
Ni kweli isiyopingika kabisa, kwamba MKONO WA MUNGU UMEKUFANIKISHA SANA kwenye huduma, biashara, kazi, lakini pia ni UKWELI USIOPIGINGIKA KWAMBA UNAYO 'LAKINI' INAKUTESA.
UONGO unakutesa... 
UZINZI unakutesa... 
KUANGALIA PICHA/VIDEO CHAFU (Pornography) zinakutesa... 
HASIRA iliyopitiliza inakutesa (Ukikasirika mpaka unatetemeka na kumkosea Mungu).
KUJICHUA kunakutesa...
TAMAA zinakutesa... 
DHAMBI zinakutesa... 
Addictions mbalimbali zinakutesa.... 
Watu wanakuona UNA HESHIMA KUBWA, na ni kweli kabisa KUNA MAENEO AMBAYO UNA HESHIMA, LAKINI HIYO HESHIMA HAIKUONDOLEI UKOMA. Mafanikio yako yameshindwa kabisa kuiondoa 'LAKINI' yako. 
Wengine wanazificha "LAKINI" zao kwa kisingizio cha "Mungu anajua sisi ni wadhaifu" au "Mungu ni Mwenye Rehema" au "Mungu ni mwenye Neema nyingi".
Nakubaliana kabisa kwamba, kweli sisi ni wadhaifu, lakini Mungu anayeishi ndani yetu si mdhaifu, hilo tu linatufanya tusiwe dhaifu. Kwa hiyo, TUNAYAWEZA YOTE KATIKA YEYE KRISTO ALIYE NDANI YETU. 
Ni kweli, Mungu ni mwenye rehema, ni kweli Mungu ni mwenye Neema, NDIO MAANA AKAMLETEA NAAMANI MTU AMBAYE ATAMUELEKEZA KWA MTUMISHI WA MUNGU ATAKAYEMSAIDIA. Ndio maana amekuletea ujumbe huu (utumike kama mjakazi alivyotumwa kwa Naamani). Ndio maana hujaangamia katika LAKINI yako. Ndio maana mpaka sasa bado wapo WATUMISHI WENYE NGUVU ZA MUNGU kumsaidia aliyekwama kuvuka.
Kitendo cha Naamini kujaribu mbinu zote akashindwa, haimaanishi kwamba UKOMA hauwezi kabisa kutakasika.
Ile kwamba umejaribu kufunga, kuomba na kufanya juhudi zako binafsi ikashindikana, haimaanishi DHAMBI HIYO HAIWEZEKANI.
Lakini ya Naamini ilimuhitaji NABII WA MUNGU. Ilimuhitaji Mtu mwenye nguvu za Mungu amsaidie. Haikuhitaji fedha, heshima wala umaarufu, ilihitaji NGUVU. 
Hizo dhambi na addictions ambazo zinakutesa ZINAMUHITAJI MTU MWENYE NGUVU ZA MUNGU. Zinakuhitaji KUIVUA HESHIMA yako na kuamua kwa dhati kupata msaada. 
Mmoja wa wana wa manabii aliyeenda kukata miti pamoja na Nabii Eliya, baada ya kuigundua 'LAKINI YAKE', yaani shoka KUDUMBUKIA, akalia kwa sauti akisema "Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile."
2 Wafalme 6:5 Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.
Nabii Isaya, baada ya kugundua 'LAKINI YAKE' ni midomo michafu (matusi, uongo, uzushi, usengenyaji nk), hakukaa kimya, alivua heshima yake na akalia kwa sauti kuu akisema "Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu" 
Isaya 6:5 Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi.
Paulo akasema, katika Warumi 7:24 "Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?" 
Lakini hakuishia hapo, bali akaendelea kusema "Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu." Warumi 7:25
Ashukuriwe Mungu kwa ajili ya mjakazi wa mke wa Naamani aliyemuunganisha na Nabii Elisha.
Ashukuriwe Mungu kwa watumishi wa Mungu waliopakwa mafuta kushughulika na LAKINI zetu. 
Unaposoma ujumbe huu, Ujumbe huu utumike kama Mjakazi wa Naamani, na Roho Mtakatifu akuelekeze mahali sahihi pa kupata msaada wa hiyo 'LAKINI' iliyokutesa siku nyingi.
Neno la Mungu linasema katika Mithali 28:13 "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema." 
Lakini pia linatuonya katika Waebrania 12:1b "na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu" 
Mzee Yakobo, kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu anasisitiza na kusema 
Yakobo 5:16 "Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa." 
Usikubali kufa na LAKINI yako, WAKATI MSAADA UPO NA UHURU WA KWELI UPO.

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

#Umebarikiwa

~Na Mwl. Francis M. Langula

+255754711247

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!