Text

Mchanganyiko Maalum Unaomchanganya Shetani na Watumishi Wake

1 views 1 day ago

“Yohana 14:20

Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.”

Katika maandiko hayo niliyonukuu, Yesu anasema maneno yenye nguvu sana ambayo ninaamini wanafunzi wake tukiyaelewa yatatuzalishia ujasiri wa hali ya juu sana.

Anawaambia wanafunzi wake, SIKU ILE MTATAMBUA MCHANGANYIKO HUU MAALUM SANA.

Ukifuatilia maandiko yanayotangulia utagundua Yesu anaposema SIKU ILE anamaanisha WATAKAPOMPOKEA ROHO MTAKATIFU.

Yesu akiwa amekaribia kupaa kwenda kwa BABA, anasema, baada ya muda mfupi ULIMWENGU HAUTANIONA, kwa sababu ataondoka katika Mwili wa nyama na ninaenda kwa Baba, lakini anaongezea kusema LAKINI NINYI (Wanafunzi wangu) MTANIONA (Sio kwa macho ya nyama bali kwa imani kupitia Roho Mtakatifu), halafu anaongeza kusema na kwakuwa MIMI NIKO HAI NANYI MTAKUWA HAI.

Yaani mkiniona KUPITIA ROHO MTAKATIFU kwa MACHO YA IMANI, UHAI WANGU UTAHAMIA KWENU.

Yaani Roho Mtakatifu atasababisha uhai au uzima wangu uwe ndani yenu, au kwa lugha nyingine Roho Mtakatifu ndio Uhai wangu ndani yenu.

“After a little while the world will no longer see Me, but you will see Me; because I live, you will live also.” JOHN 14:19 AMP

“Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.” Yohana 14:19 SUV

Kimsingi anachosema Yesu hapa, kwa kuja kwa Roho Mtakatifu katika maisha yetu, baada ya Yeye kuondoka katika mwili, KUTATOKEA MCHANGANYIKO MAALUMU WA UHAI, KATI YETU SISI WANAFUNZI WAKE, YESU MWENYEWE NA MUNGU BABA. Kwa sababu, ukifiatilia utagundua ni baada ya kumtambulisha Roho Mtakatifu ndipo Yesu anaanza kuelezea huu mchanganyiko maalum.

Roho Mtakatifu atasababisha uhai wetu uchukuliwe na uhai wa Yesu na Yesu atupatie uhai wake, au UZIMA WAKE.

Paulo ameeleza pia kwenye

Wagalatia 2:20 “Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”

Anasema, uhai nilionao sasa KATIKA MWILI (sio katika roho tu), UNATOKANA NA IMANI NILIYONAYO KATIKA YESU.

Na kwa msingi tulioweka hapo juu, imani hiyo ni ile ambayo itamdhihirisha Yesu kupitia kumpokea Roho Mtakatifu.

Sasa, katika mistari tunayotafakari ya

Yohana 14:20 “Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.”

Yesu anaweka wazi ni KITU GANI ROHO MTAKATIFU ANAFANYA NDANI YETU.

Yaani anaeleza NI MCHANGANYIKO GANI MAALUM UNATOKEA TUNAPOMPOKEA ROHO MTAKATIFU.

Kabla sijaendelea, ni vizuri tutambue kwamba MCHANGANYIKO HUU MAALUMU UNATOKEA (UNAFANYIKA) NDANI YETU NA SIO MBINGUNI.

Yesu ndani ya Mungu Baba NDANI YETU, na Sisi ndani ya Yesu, na Yesu ndani yetu, YOTE HAYO NI NDANI YETU KUPITIA ROHO MTAKATIFU.

Uhai wetu umefichwa ndani ya Yesu, na Yesu ndani ya Mungu na wakati huo huo Yesu yuko ndani Yetu sisi kupitia Roho wa Mungu.

Hata kama huielewi, imeze hivyo hivyo ilivyo na itafanya kazi tu. Haya ni mambo ya Rohoni, akili inaweza isielewe.

Wakolosai 3:3 “Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.”

Kwenye Wakolosai, Paulo amejaribu kuelezea, anasema SISI TULIKUFA, NA UHAI WETU UMEFICHWA PAMOJA NA KRISTO NDANI YA MUNGU, kimsingi anaeleza kitu kile kile tunachotafakari.

Kama kuna kitu kinamchanganya Shetani, mapepo yake, wachawi, waganga na watumishi wake, basi ni HUU MCHANGANYIKO MAALUMU NDANI YETU.

Wachawi, waganga na watumishi wa Shetani wanatuona kama watu wa kawaida, wakati mwingine tunakutana nao mtaani, tuko nao makazini, tunafanya nao biashara bila sisi kujua, LAKINI WAKITAKA KUTUROGA WANAONA SIO SISI TENA.

Wanapojipanga kuja kichawi, wakati wanakuja, Yesu ndani yangu kupitia Roho Mtakatifu anatokeza nje yangu na mimi ninarudi ndani, wanatarajia wanikute mimi, wanamkuta Yesu, uchawi wao unakwama.

Wakati ninapanga safari wananiona mimi naenda kupanda basi, bodaboda, ndege au usafiri wowote ninaotumia, WAKITUMA MAPEPO YA AJALI, wanashangaa mimi sipo, Yesu anajidhihirisha na jeshi la malaika walinzi.

Kweli hii ya Neno la Mungu ikupe ujasiri na iinue imani yako.

Sio mimi ninayeishi bali ni Yesu ndani yangu.

MIMI NI MCHANGANYIKO MAALUM UNAOMCHANGANYA SHETANI NA WATUMISHI WAKE.

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

Umebarikiwa

~Na. Mwl. Francis M. Langula

(+255754711247)

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!