Text

Mtazamo Sahihi Ili Kushinda Kila Aina ya Changamoto Au Jaribu

1 views 1 day ago

2 Wakorintho 4:17

“Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda mfupi tu, yatuandalia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;”

Neno hili la tafakari ya leo limetaja maneno matatu ya muhimu sana sana.

1) Nyepesi

2) Ya muda mfupi

3) Yatuandalia utukufu

Mtu anapopita katika dhiki fulani au changamoto fulani, moja ya kitu kitakachomsaidia kupata ushindi ni kuwa na mtazamo sahihi katika kipindi cha mateso au dhiki!

Watu wengi majaribu yamekuwa yakiwamaliza sio kwa sababu ya UKUBWA wa jaribu bali kwa sababu ya MTAZAMO USIO SAHIHI!

Kimsingi hakuna jaribu kubwa sana au dogo sana kwa asili yake, UKUBWA au UDOGO utategemea mtazamo wa muhusika!

Ndio maana jaribu aina moja linaweza kuwapata watu wawili tofauti, mmoja likamuangusha na mwingine akashinda na kupita salama kwa ushindi, kwa hiyo shida haiko kwenye jaribu bali kwa mjaribiwa!

Jaribu ni sawa kabisa na PUSH UP (au zoezi lingine lolote), kwa mtu, mmoja yaweza kuwa ADHABU (itakayozalisha manung'uniko) lakini kwa mtu mwingine MAZOEZI ya kujenga mwili (yanayofanywa kwa furaha)

Kinachoifanya PUSH UP kuwa adhabu na mateso ni mtazamo na utayari wa muhusika!

Sasa baada ya maelezo hayo turudi kwenye andiko letu, "Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda mfupi tu, yatuandalia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana"

Ukiangalia kwa haraka haraka unaweza ku     dhani Paulo alikuwa na dhiki nyepesi tu ndio maana akaandika maneno hayo, lakini ukifuatilia utagundua hakuwa na dhiki nyepesi.... unaweza ukasoma 2 Korintho 4 kuanzia mstari wa 7 ukaenda mpaka 2 Korintho 5:4

Nitaweka mistari kadhaa hapa chini uone hii dhiki haikuwa nyepesi kwa asili yake

“twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twabeba katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.” 2 Wakorintho 4:9-10 SUV

“Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi. Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu, aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kuwa atazidi kutuokoa;” 2 Wakorintho 1:8-10 SUV

“Kwa maana hata tulipokuwa tumefika Makedonia miili yetu haikupata nafuu; bali tuliteseka kotekote; nje palikuwa na vita, ndani hofu.” 2 Wakorintho 7:5 SUV

Nafikiri kwa maandiko hayo unaweza kuelewa sasa ninachokizungumza... yaani Paulo alikuwa kwenye dhiki iliyo hatarisha maisha yake kwa kifo, lakini iliyosababisha hofu ndani yake, iliyosababisha kulemewa kuliko nguvu zake, iliyomfanya afikiri atakufa....

Kwa kiasi cha dhiki alichopitia, ninaamini kabisa kwa andiko hili tunalotafakari leo, Paulo alikuwa anafunua siri za ushindi wa majaribu hayo ali     yopitia...

Na siri yenyewe iko kwenye maneno hayo matatu aliyoyasema kwenye andiko letu la tafakari, 2 Kor 4:17 Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda mfupi tu, yatuandalia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;

Ninaamini hata kama uko katika dhiki au changamoto ya aina gani, ukiwa na mtazamo huu utavuka salama na kwa ushindi!

Jiambie mwenyewe:-

1) HII DHIKI AU CHANGAMOTO NINAYOPITIA NI NYEPESI

Kujiambia na kujiaminisha kuwa changamoto yako ni nyepesi ni sawa kabisa na kujipa uwezo wa kuikabili na kuimudu.

Ukweli ni kwamba ili dhiki hiyo kukupata au kunipata ni ishara kwamba ninaimudu

“Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita muwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili muweze kustahimili.” 1 Wakorintho 10:13

Shetani hupenda kutuonyesha ukubwa wa changamoto ili kutusahaulisha ukuu wa Mungu!

Wepesi wa changamoto au ugumu wake hauko kw     enye changamoto, bali uko kwenye mtazamo wa muhusika, usiitazame changamoto, MTAZAME MUNGU NA NENO LAKE LINASEMA NINI KWA CHANGAMOTO ZA AINA HIYO, kwa kufanya hivyo utaweka wepesi wa kuikabili changamoto!

2) HII DHIKI NINAYOPITIA NI YA MUDA, sio ya milele, kama ilivyoanza lazima itaisha.

Sasa ujue shetani pia anaijua silaha hii, kwa hiyo siku zote huwa anajaribu kutuonyesha kwamba changamoto zetu zitadumu milele na zitatumaliza... lakini UKWELI NI KWAMBA DHIKI YETU NI YA MUDA TU!

Shetani hutushawishi kwamba dhiki tunayopitia ni ya kudumu ili KUWEKA SHINIKIZO (PRESSURE) NDANI YETU KUJITOA KWENYE CHANGAMOTO KWA NJIA YOYOTE ILE na kwa kufanya hivyo tunaweza kujikuta tumeharibu!

Lakini pia silaha hii shetani huitumia KUONDOA AMANI NA UTULIVU NDANI YETU KIPINDI CHA CHANGAMOTO.

Lakini huweza kusababisha tukawapa shinikizo (pressurerize) wanadamu kutusaidia kiasi ambacho wasipofanya sawa na shinikizo tunalowapa ikasababisha magomvi!

Tulia na ujiambie mpaka uelewe, kwamba DHIKI HII NINAYOPITIA SIO YA MILELE, NI YA KITAMBO KIFUPI TU, MOYO WANGU TULIA USIWE NA PAPARA...

Lazima tujifunze KUZISEMESHA NAFSI ZETU ZITULIE WAKATI MUNGU ANATUVUSHA...

Moja ya sifa ya sauti ya adui, ni lile shinikizo (pressure) linalokuwa nyuma ya ile sauti likiambatana na hofu.

“Ee nafsi yangu, urudi pumzikoni mwako, Kwa kuwa BWANA amekutendea ukarimu.” Zaburi 116:7 SUV

“Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote.” Zaburi 103:2 SUV

3) HII DHIKI NINAYOPITIA, HUNIFANYIA UTUKUFU!

Jiambie mpaka uelewe kwamba, NIKIVUKA SALAMA NITATOKA KAMA DHAHABU...

Nikivuka kwa ushindi itaniongezea UTUKUFU NA HESHIMA...

Nitavikwa taji ya ushindi mbinguni...

“Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji la uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao.” Yakobo 1:12 SUV

Sote tunapenda TAJI, lakini tunasahau ASTAHIMILIYE MAJARIBU NDIO HUVIKWA TAJI!

Ninaamini ukijijengea mtazao sahihi kwenye maeneo hayo matatu, ITAKUSAIDIA SANA KUVUKA KWA USHINDI KILA JARIBU.

JIAMBIE DHIKI HII INANIONGEZEA THAMANI KAMA VILE MOTO UNAVY     OIONGEZEA DHAHABU THAMANI!

Kanuni hii inafanya kazi hata kwenye maumivu mbalimbali mtu anayoweza kukutana nayo, yaweza kuwa maumivu ya mwili (physical pain) au maumivu ya nafsi au hisia (emotional pain)

Katika hali ya maumivu, jiambie na kujielewesha mambo haya matatu na utashangaa ukali wa maumivu unapungua kwa asilimia kubwa.

- Maumivu haya ni ya muda tu (This pain is temporary) kwa hiyo hakuna uharaka wowote (There is no urgency)

- Ninao uwezo wa kutosha kuyamudu.

- Nitatoka na ushindi, nitayashinda na yatanifanya kuwa imara zaidi (I will come out stronger)

HAHUNA CHA KUKATA TAMAA, SHETANI ATASUBIRI SANA TUKATE TAMAA, HATUKATI TAMAA NG'O.

KUSHINDA NI LAZIMA NA KUVUKA KWA USHINDI NI LAZIMA, HAKUNA NAMNA.

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

Umebarikiwa

~Na. Mwl. Francis M. Langula

(+255754711247)

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!