Mtwike Yesu Fadhaa na Masumbufu yako
1 Petro 5:7 SUV
"huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
Tunamtwika Yesu fadhaa zetu, wasiwasi wetu, huzuni zetu na mahangaiko yetu kwa njia ya maombi yetu, na tunafanya hivyo kwa sababu Yeye, YESU anajishughulisha sana na mambo yetu.
Yaani kama mambo yetu hayaendi sawa kiasi cha kutusumbua, yeye YESU anatamani tumpatie hayo masumbufu tunayoyapitia.
Yesu anajihusisha sana na mambo yetu
Tatizo letu ni kuwa tunamtwika kwa njia ya maombi halafu tunabaki tumebeba mzigo wa mahangaiko kwa jambo hilo hilo tulilomtwika Yesu.
Kuanzia leo, kila unapoombea jambo, hakikisha hauondoki kwenye maombi au huachi kuliombea mpaka uwe na uhakika mzigo wako amechukua Yesu na wewe unaondoka ukiwa huru
Sio sahihi kuendelea kubeba mzigo ambao Yesu yuko tayari kukubebea.
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Wafilipi 4:6-7 SUV
Usikubali kusumbukia neno lolote; kila linalokusumbua, hakikisha unalipeleka madhabahuni kwa sala, maombi na shukrani na usiondoke hapo mpaka mambo mawili yamekutokea
1. Umekuwa na uhakika hiyo haja yako iliyokuwa inakusumbua imejulikana na Mungu.
2. Amani ya Kristo imekuhifadhi moyo na nia yako.
Ikiwa inamaana kuwa, fadhaa na mahangaiko yako yameondoka ndani yako na badala yake umejaa amani.
Kumbuka: Kwenye maombi ni mahali pa mabadilishano (a place of exchange). Unampa Yesu masumbufu na fadhaa zako anakupa Amani yake
Hii amani inakuhifadhi muda wote unaposubiri udhihirisho wa majibu ya maombi yako.
Amani hiyo ni kiashirio kuwa jibu lako limeshaachiliwa.
Japokuwa inawezekana haujapokea kile ukiombacho, lakini amani itauhifadhi moyo wako usiharibiwe katika kusubiri kupokea kama vile chumvi inavyohifadhi chakula kisiharibike.
“Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.” Isaya 26:3 SUV
Kama hujabadilishana fadhaa yako na amani ya YESU, usitoke kwenye maombi au usiache kuliombea jambo hilo. Usikubali kuendelea kubeba fadhaa ambazo Yesu yuko tayari kukubebea.
Baada ya kuongelea maombi, sala na shukrani, mistari inayofuata inasema hivi:
“Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Wafilipi 4:8 SUV
Ikiwa na maana kuwa, Baada ya kufanya mabadilishano na YESU akakupa amani, kuwa makini unatafakari nini.
CHOCHOTE AMBACHO HAKIANGUKII KWENYE WAFILIPI 4:8 KUHUSIANA NA JAMBO HILO AMBALO UMEMTWIKA YESU. USIKUBALI KUKITAFAKARI.
Kwa jinsi hiyo uta secure kila ombi lako mpaka unapokea udhihirisho wa majibu yako.
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mw. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author