Mwili Usiotolewa Kwa Mungu Kama Dhabihu Umebeba Mauti
Warumi 7:24 SUV
“Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?”
Mwili ni mzuri sana lakini usipotolewa kwa Mungu kikamilifu, unaweza kusababisha madhara makubwa ya roho na nafsi ya Mwanadamu!
Kwenye andiko hapo juu, Neno limeuliza, NI NANI ATAKAYENIOKOA NA MWILI HUU WA MAUTI?
Maana yake kwenye mwili wa mwanadamu iko mauti ya roho!
Kwa hiyo, anayefanya mchezo na mwili wake, anaweza kabisa kujisababishia mauti ya milele Jehanam!
Neno la Mungu linaongeza kusema kuwa "Nia ya Mwili ni mauti"
“Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani.” Warumi 8:6 SUV
Kwa hiyo, mwili unavutia upande wa mauti na uharibifu!
Ndio maana Neno pia linasema
“Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Wagalatia 5:19-21 SUV
Kwa hiyo, mwili ukiachiwa, utakuwa mwepesi kabisa kuyatenda hayo yaliyotajwa hapo juu pamoja na yote yafananayo na hayo!
Lakini kitu cha ajabu ni kwamba, SIKU YA HUKUMU MUNGU ATATUHUKUMU KWA YALE TULIYOFANYA KATIKA MWILI, Hiyo inadhihirisha umuhimu wa HUU MWILI KATIKA KUAMUA MAISHA YETU YA SASA NA YA MILELE BAADA YA DUNIA HII!
Angalia andiko hili:-
“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” 2 Wakorintho 5:10 SUV
Ndio maana Neno linasisitiza kuwa
“Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake;” Warumi 6:12 SUV
Maana yake ni kwamba mwili unaweza kabisa kukusababishia mauti!
YESU PIA ALIUVAA MWILI WA AINA HII HII KAMA WETU, maana ilimpasa kama kuhani afananishwe na sisi ili sadaka ya dhambi kwa ajili yetu iwe halali kisheria!
“Yeye [yaani Yesu], siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii;” Waebrania 5:7, 9 SUV
Yesu alijua amevaa mwili wa mauti, mwili ambao una asili ya dhambi na mauti ndani yake kwa sababu ya anguko la Adam, AKAMTOLEA MUNGU [AMBAYE ANAWEZA KUMUOKOA NA MWILI WA MAUTI] MWILI WAKE MPAKA AKAKAMILISHWA na ndipo akawa SABABU YA WOKOVU WETU!
Yesu alitoa mwili wake kwa MAOMBI (YA MIKESHA PAMOJA NA KUFUNGA), DUA (MAOMBI MAALUMU YA KUUTIISHA MWILI), KULIA SANA NA MACHOZI; Naye akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu! Na ndipo MWILI WAKE SASA ULIKUWA DHABIHU MBELE ZA MUNGU NA UKAWA SABABU YA WOKOVU WETU SOTE!
“Kwa hiyo [YESU] ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.” Waebrania 10:5-7, 10
Vivyo hivyo na sisi, KWA MAKUSUDI KABISA NI LAZIMA TUITOE MIILI YETU DHABIHU MBELE ZA MUNGU ILI MUNGU AITUMIE KWA UTUKUFU WAKE!
NI LAZIMA TUKUBALI KUYAUA MAPENZI YA MIILI YETU NA TAMAA ZAKE ILI UZIMA WA KRISTO NA NGUVU ZA MUNGU ZIPITE KWENYE MIILI YETU!
“Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.” 2 Wakorintho 4:11 SUV
Ili Mungu afanye kazi hapa duniani anahitaji mwili, na ndio maana ALIINUNUA MIILI YETU KWA DAMU YA T HAMANI YA MWANAE YESU.
“Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu” 1 Wakorintho 6:19-20 SUV
Mungu alinunua miili yetu kwa sababu Yeye ni Roho, na ili afanye kazi duniani anahitaji MWILI autumie!
Pamoja na kwamba miili Yetu ni Hekalu la Mungu, lakini MUNGU HAYUKO TAYARI KUCHANGIA HEKALU HILI NA SHETANI!
“Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!” 1 Wakorintho 6:15 SUV
Kwa hiyo MUNGU HAYUKO TAYARI KUUTUMIA MWILI AMBAO HAUJATOLEWA KWAKE KWA ASILIMIA 100!
Na kama hatujaitoa miili yetu kwa Mungu maana yake ni kwamba, MAUTI IKO NDANI YA MIILI YETU!
Ni Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuokoa miili yetu na mauti (dhambi), lakini atauokoa mwili uliotolewa kwake tu!
Watu wengi dhambi inawashinda sio kwa sababu dhambi ina nguvu sana ila ni kwasababu hawajaitoa MIILI YAO kwa MUNGU kwa asilimia 100!
Sehemu yoyote ya Mwili ambayo hujaikabidhi kwa Mungu 100% kwa kumaanisha, maana yake umeikabidhi kwa dhambi na mauti (shetani)!
Ndio maana Paulo akatusihi sana akisema
“Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Warumi 12:1 SUV
Mungu anataka miili yetu tukiwa hai, dhabihu hai. Sio mpaka tufe
Ili ibada zetu ziwe na maana na tumpendeze Mungu ni lazima TUAMUE KUMPATIA MUNGU MIILI YETU!
Huo mwili sio mali yako mwenyewe ni mali ya Mungu, mpatie autumie kwa utukufu wake!
Kumbuka: Mungu atatuhukumu kwa jinsi tulivyoitumia miili yetu!
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author