na Ahimidiwe Bwana; Asiyetutoa Kuwa Mawindo (Mateka) Kwa Changamoto Tunazopitia
Zaburi 124:6-8 SUV
“Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.”
Kuna hali za maisha ambazo tunaweza kuzipitia zikaonekana kama zinatutafuna na kutumaliza.
Lakini Neno la Mungu linasema wazi, Mungu hawezi kututoa kuwa mawindo au mateka kwa meno ya hali ambazo ni kama zinataka kutumaliza.
Ukisoma hii Zaburi 124:1-5 utakutana na maneno yafuatayo;
“Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo.” Zaburi 124:2-5 SUV
Kusudi la adui halikuwa kukutisha tu au kukuumiza tu bali alitaka AKUMEZE HAI, alitaka MAJI (CHANGAMOTO) YAKUGHARIKISHE, alitaka akumalize kiroho kabisa!
Kama si BWANA KUWA PAMOJA NAWE KATIKATI YA CHANGAMOTO HIYO, ADUI ANGEKUMALIZA KABISA MAANA HILO NDIO KUSUDI LAKE KUU!
Ile kwamba uko salama, ile kwamba huo ugonjwa haukukumaliza, ile kwamba ndani yako bado unahisi kumpenda Mungu pamoja na yote hayo, ile kwamba bado ndani yako unatamani kumpendeza Mungu japokuwa ulianguka, hiyo ni ISHARA TOSHA KWAMBA MKONO WA MUNGU UKO NAWE KUKUSAIDIA, KUKUVUSHA na KUKUINUA TENA!
Ndio maana Neno linasema: “Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji, Mtego umevunjika, nasi tumeokoka. Msaada wetu u katika jina la BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.” Zaburi 124:6-8 SUV
Chukua dakika kadhaa umshukuru Mungu kwa sababu HAKUKUTOA KUWA MATEKA KWA HIYO CHANGAMOTO KIASI CHA HIYO HALI KUKUMALIZA NA KUKUTAFUNA!
Nafsi yako itaokoka, mtego utavunjika nawe utaokoka maana msaada wako u katika Jina la Bwana!
Sio kila moto unateketeza, MIOTO MINGINE INASAFISHA NA KUNG'ARISHA!
“Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.” Ayubu 23:10 SUV
Sio kila mtu hugharikishwa na maji mengi, walioko ndani ya safina, maji hayo hayo huwafanya kuelea!
“Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.” Isaya 43:2 SUV
Maadamu Mungu yuko pamoja nawe, maji hayatakugharikisha bali yatakufanya uelee, moto hautakuteketeza bali utakung'arisha kama dhahabu! Moto utakutofautisha na watu wa kawaida, utakupandisha thamani ukivuka kwa ushindi!
Yuko mtu wa nne kwenye hilo tanuru; kama vile kipindi cha Shedrak, Meshak na Abednego; ambaye atahakikisha MOTO HAUKUTEKETEZI!
Kwa kweli, Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao! Maana Kama si BWANA aliyekuwa pamoja nasi, Wanadamu walipotushambulia. Papo hapo wangalitumeza hai, Hasira yao ilipowaka juu yetu Papo hapo maji yangalitugharikisha, Mto ungalipita juu ya roho zetu; Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo.
Usiogope hayo mapito hayatakumaliza, usiogope hizo fitina na mashambulizi kazini, haziwezi kukumaliza, usiogope hata kama UMEFUKUZWA kazi, Mungu hana chanzo kimoja cha kukutana na mahitaji yako! MUNGU HAWEZI KUKUTOA KUWA MATEKA KWA MENO YA HIYO HALI ILI YAKUMALIZE KWA SABABU "Yeye aijua njia uiendayo; Akisha kukujaribu, utatoka kama dhahabu.”
“Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.” ZAB. 37:25 SUV
Mungu hataanzia kwako kuwaacha wenye haki, kama Daudi hajawahi kuona mwenye haki ameachwa, hata wewe hautaachwa!
Hajakuacha na wala hatakuacha, atakukumbuka tu kama alivyomkumbuka Nuhu
“Na Mungu akamkumbuka Nuhu, na kila kilicho hai, na wanyama wote waliokuwamo pamoja naye katika safina; Mungu akavumisha upepo juu ya nchi, maji yakapungua;” Mwanzo 8:1 SUV
Na ahimidiwe BWANA; Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao
Usiogope, wewe sio mateka wa hiyo CHANGAMOTO, MUNGU ATAKUVUSHA LAZIMA!
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author