Neno la Mungu ni Halisia
1 Yohana 1:1 “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;”
Kwenye andiko hilo kuna mambo kadhaa ya kujifunza kuhusu Neno la uzima (Neno la Mungu).
Kuna maneno kama manne hivi muhimu sana katika andiko hili.
--Tulilolisikia
--Tuliloliona kwa macho
--Tulilolitazama
--Tukalipapasa kwa mikono
Sasa wote tunafahamu Neno la Mungu ni la rohoni lakini Yohana anasema linasikika, linaonekana, linatazamika kwa macho.
Hivi vitu vilivyotajwa hapo ni vitu vya mwilini, kusikia, kuona, kutazama na kupapasa ni vitu ambavyo milango mitano ya fahamu inahusika.
Kazi ya milango mitano ya fahamu ni kugusa, kuona, kusikia, kunusa na kuonja. Sasa Neno la Rohoni linasikika, linaonekana kwa macho linapapasika (linagusika) kwa mikono, hii ni ajabu.
Ukisoma Yohana 1:1,3 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”
Unaona, ametaja Neno alikuwa au ni Mungu (Roho), lakini pia ametaja Vitu vyote vilifanyika kupitia huyo Neno. Kwa hiyo, uwepo wa kila kitu duniani ni kwa sababu ya huyo Neno.
Kwa hiyo ni sawa kabisa na kusema "Hapo mwanzo kulikuwako Neno, na vitu vyote vilikuwa ndani ya Neno, na vitu vyote vilitokana na Neno."
Lakini pia andiko lingine linasema
Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
Sio tu kwamba Neno lilifanya vitu bali pia Neno likafanyika mwili. Yaani lilipitia mchakato fulani kufanyika Mwili unaoonekana kwa macho.
Ninachotaka tuone ni kwamba, pamoja na kwamba Neno ni la Rohoni, linavyo vitu vya mwilini ndani yake, na linao uwezo ndani yake wa kufanyika mwili.
Kwa hiyo Neno la Mungu ni SAUTI INAYOSIKIKA WAZI, ndani yake kuna uhalisia na linaweza kufanyika KITU HALISI KINACHOONEKANA KWA MACHO, KINACHOTAZAMIKA NA KINACHOSHIKIKA KWA MIKONO YA NYAMA.
Mungu akikupa Neno amekupa kila unachohitaji, ukiliamini na kufanyia kazi maelekezo yake na kulishika bila kukata tamaa, utaliona likiwa halisi kwenye maisha.
Mimi binafsi, Roho Mtakatifu akinilitea Neno ndani yangu kuhusu jambo fulani, au ninaposoma Biblia, nikigundua Neno linalohusu changamoto au jambo fulani, kwa kweli napata ujasiri na naanza kulifuatilia hilo Neno na kuliamini kuliko hata uhalisia wa jambo ninalopitia.
Neno la Mungu linaweza kushughulikia kila uhitaji wa vitu tulionao kwa sababu VITU VYOTE vilofanyika kwa Neno. Kwa hiyo Neno la Mungu ni jibu la uhitaji wa AFYA, FEDHA, KAZI, BIASHARA, HUDUMA nk.
Unapokutana na changamoto jambo la kwanza unalohitaji ni NENO LA MUNGU kuhusiana na hiyo changamoto, unaweza ukaamua kwenda kwenye maandiko na kumwambia Roho Mtakatifu akuongoze Neno sahihi, lakini pia Roho Mtakatifu anaweza akakupatia (akakukumbusha) Neno ndani yako. Roho Mtakatifu akikupatia Neno, (kwa njia yoyote ile) anza kulisoma na Kujifunza (Study) hilo Neno, mpaka USIKIE au UDAKE SAUTI ILIYO KATIKA HILO NENO (SAUTI YA NENO) upate na MAAGIZO KATIKA HILO NENO, baada ya hayo AMUA KULIAMINI na KUANZA kuyafanyia kazi Maagizo YA NENO, na uling'ang'anie MWISHO UTAONA MATOKEO.
Zaburi 103:20 “Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake.”
Ili Neno lifanyike HALISI KWENYE MAISHA YAKO, kuna vitu viwili lazima uvidake kwenye Neno;
Moja, ni Sauti Ya Neno na mbili ni Maagizo ya Neno. Ni lazima UJUE NENO LINAKUELEKEZA UTENDE NINI.
Nguvu iko kwenye kuisikia SAUTI kwenye Neno na KULITENDA NENO.
Yakobo 1: 22 – 23 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.”
Neno linalofanyika mwili kwako ni lile ambalo UMEGUNDUA CHA KUTENDA KUTOKA KWAKE NA UMEANZA KUKITENDA.
Ukiwa unasoma Neno la Mungu, ukisikia maagizo ya Neno na ukaona jambo la kufanya kupitia Neno, na ukawa mwaminifu kulifanya, hilo Neno halitapotea, lazima LITAFANIKIWA.
Mathayo 7:24,26 "Basi kila ASIKIAYE hayo maneno yangu, NA KUYAFANYA, atafananishwa na MTU MWENYE AKILI,”
Yakobo 1:25 “Lakini aliyeitazama sheria kamilifu [NENO LA MUNGU] iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.”
Isaya 55:11 “ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”
Neno la Mungu lazima LITAFANIKIWA kwa mtu ambaye ATALIPOKEA NA KULIFANYIA KAZI. Haliwezi kabisa kumfelisha mtu.
Neno la Mungu linasikika, linaonekana, matendo yake yanaonekana, linashikika. Ukiamua KULIAMINI KULIKO KINGINE CHOCHOTE, UKIAMUA KILITENDEA KAZI, NI HALISI na haiwezekani lisizalishe matokeo. Linaanzia rohoni lakini linaweza KUFANYIKA MWILI ukaona, ukasikia, ukashika na kutazama matokeo yake.
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa
~Na Mwl. Francis M. Langula
+255754711247
Mwl. Francis Langula
Author