Text

Ni Ndoto Tu

1 views 1 day ago

Mwanzo 41:7 – 8

Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; 

Habari hii ya ndoto ya Farao imenifanya nijiulize sana kuhusu ndoto. 

Mara kadhaa nimekutana na watu ambao wamekutana na matukio na wakati wanaelezea matukio wanasema kabla ya tukio niliota na nikadhani "NI NDOTO TU", lakini kumbe HAIKUWA NDOTO TU BALI UJUMBE AMBAO ULITAKIWA KUFANYIWA KAZI. 

Farao pia, baada ya kuota ndoto hiyo alidhani NI NDOTO TU isiyo na maana yoyote lakini kilichomsaidia ni roho yake kufadhaika baada ya kuamka. 

Nataka ninukuuu habari yote ya ndoto hiyo hapa chini kisha nitaendelea.

Mwanzo 41:1-8 Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto. Na tazama, ng’ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini. Na tazama, ng’ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng’ombe wengine ukingoni mwa mto. Kisha hao ng’ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng’ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka. Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema. Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao. Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu. Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.

Mungu alimletea Farao ujumbe mkubwa kwa ndoto. Mungu alikusudia kuiponya Misri na nchi za jirani kupitia UJUMBE WA NDOTO, Mungu alikusudia KUMUINUA YUSUFU kupitia ujumbe wa Ndoto. 

Jaribu kufikiri Farao angeendelea kulishika lile wazo la NI NDOTO TU na kuipuuzia pia sauti ya roho yake baada ya kutoka kwenye ndoto. Miaka saba ya Shibe ingekuja na wangetumia vibaya na kufuja (misuse) chakula ambacho kilitakiwa kuhifadhiwa vizuri kwa ajili ya baadaye.

Na Baadaye miaka saba njaa kali ingeanza na wangeanza kujutia chakula walichoharibu na wengi sana wangekufa na njaa sio tu Wamisri lakini pia hata nchi za jirani.

Kama Farao asingefanyia kazi UJUMBE WA MUNGU kupitia ndoto, Yusufu asingepata fursa ya Kutafsiri ndoto na kupitia tafsiri kupandishwa cheo kuwa waziri mkuu. 

Farao angeendelea kufikiri NI NDOTO TU angesababisha maafa makubwa.

Kuna watu wengi Mungu amewaonya kwa njia ya ndoto na wakapuuzia wakidhani NI NDOTO TU na matokeo yake wakajikuta wamepata hasara na madhara makubwa. 

Kuna wengine wamepoteza wenzi wao, ndugu zao, jamaa zao, rafiki zao kwa kudhani NI NDOTO TU na kuzipuuzia bila kuchukua hatua.

Kuna wengine wamesababisha TAIFA LIKAINGIA KWENYE MATATIZO MAKUBWA kwa kudhani NI NDOTO TU na kuzipuuzia.

Wengine wamesababisha AJALI MBAYA ZA NDEGE, MELI, MABASI NK kutokea kwa kupuuzia kufanyia kazi UJUMBE WA MUNGU kupitia ndoto ambao walipaswa KUCHUKUA HATUA KUZUIA WALICHOKIONA.

Mungu akifunua jambo kupitia ndoto, mara nyingi kama si mara zote, anataka muhusika AFANYIE KAZI NDOTO HIYO kuzia jambo hilo lisitokee au kupunguza au kuondoa madhara ikiwa jambo litatokea. Na njia ya kuzuia ni KUCHUKULIA NDOTO KWA UMAKINI NA KUOMBA KWA UONGOZI NA MAELEKEZO YA MUNGU MWENYEWE IKIWA NI PAMOJA NA KUCHUKUA HATUA PIA.

Neno la Mungu linasema katika Ayubu 33:14-18 Kwa kuwa "Mungu hunena" mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni,  Na uhai wake usiangamie kwa upanga."

Ayubu anathibitisha kwamba, KUPITIA NDOTO, Mungu anaweza akanena na mtu mara moja hata mara mbili. Lakini pia anasema kupitia ndoto, Mungu anaweza akazuia Nafsi ya mtu isiende shimoni na uhai wake usiangamie kwa upanga.

Kupitia ndoto, Mungu alizungumza na Yusufu baba yake Yesu kwamba asimuache Mariamu mama yake Yesu. Na Kupitia ndoto, Mungu aliwaonya mamajusi wasirudi kwa Herode, Lakini pia, kupitia ndoto, Mungu alimuonya Yusufu amkimbize Yesu asiangamizwe na Herode.

Mathayo 1:20,24 Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe;

Mathayo 2:12 Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine.

Mathayo 2:13-14 Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri;

Kuna watu Mungu amewaonya wasifanye biashara fulani katika ndoto wakapuuzia na kupata madhara.

Kuna wengine Mungu amewaonya katika ndoto waache mahusiano na mtu au watu fulani na wakapuuzia na kujikuta wamepata madhara makubwa.

Kuna wengine mara nyingi wanaota wakitendewa mabaya na marafiki zao au watu wanohusiana nao kwa karibu na wanapuuzia wakisema NI NDOTO TU. Na kumbe Mungu anawaonya wachukue tahadhari na hayo mahusiano.

Kuna wengine Mungu amezungumza nao KUPITIA NDOTO wawahudumie watumishi wa Mungu na wakapuuzia wakisema NI NDOTO TU na wakapishana na majibu yao.

Wengine wamepewa Maagizo katika ndoto wawatunze yatima na wajane na wakadhani NI NDOTO TU.

Wengine kwa uwazi kabisa wanazuiliwa wasifanye maamuzi ya kuingia kwenye ndoa na mtu huyo lakini wanapuuzia na kusema NI NDOTO TU.

Ninachomaanisha sio kurukia tu kila ndoto na kufanya maamuzi (sababu hata shetani pia hupitisha vyake kwenye ndoto), point yangu ni kwamba, USIPUUZIE NDOTO UNAYOOTA, ni vizuri kuichunguza na kumuuliza Mungu, kuiombea na kuchukua hatua zinazotakiwa.

Kuliko kupuuzia ndoto na ukajikuta unapata madhara makubwa, ni bora kuchukulia uzito ndoto na KUZIFUATILIA MPAKA UWE NA UHAKIKA NDOTO HIYO HAINA MAANA au ni ya shughuli nyingi sawa na Mhubiri 5:3 "Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi;"

Zingatia Yafuatayo kutoka kwenye maandiko tuliyonukuhu kwenye somo hili kuhusu ndoto:-

(1) Mungu anatabia ya kuzungumza na watu wake kupitia ndoto, kuwafundisha, kuwaonya na hata kuwaelekeza.

(2) Mungu anaweza kuzuia maangamizo ya nafsi ya mtu, familia, jamii na hata taifa kupitia ndoto anayoileta kwa mtu

(3) Usipuuzie ndoto hata kama hujaielewa. 

(4) Zingatia ndoto zinazojirudia rudia 

-- Yaani, unalala unaota, unaamka katikati ya usiku na ukilala unaota tena ndoto ile ile au inayofanana na ile.

-- Au yaweza kuwa unaota ndoto zinazofanana hata kama zimepishana siku nyingi au chache.

-- Kujirudia kwa ndoto ni moja ya ishara kwamba jambo hilo uliloota limethibitishwa na lipo karibu sana kutokea

Mwanzo 41:32 Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

(5) Zingatia ndoto ambazo baada ya kuziota zinaifadhaisha roho yako. Kwa lugha nyingine zinakukosesha amani na kukufanya ndani yako ukose utulivu.

-- Hata kama umeota ndoto ukaisahau lakini ndani yako unakumbuka kuna ndoto uliota na inakukosesha amani.. Usipuuzie, nenda mbele za Mungu mwombe akukumbesha na kushughulika na huo ujumbe mpaka upate amani. 

(6) Usipuuze ujumbe wa kwenye ndoto zako kuhusu watu au mtu hata kama hauendani kabisa na anachokisema yule mtu au unayoyaona kwake.

Herode aliwaambia mamajusi maneno mazuri kuhusu Yesu na kusudi lake kwa Yesu lakini Mungu akaufunua uhalisia wa moyo wa Herode na kusudi lake kupitia ndoto. Usiwe mwepesi sana kuhukumu na kufanya maamuzi kutokana na ndoto lakini USIPUUZIE NA KUSEMA NI NDOTO TU, FANYIA KAZI ULICHOKIOTA.

(7) Uwe makini sana na HALI UNAYOISIKIA NDANI YAKO mara baada ya kutoka kwenye ndoto, inaweza ikakupatia mwanga kuhusiana na kile umekiota.

(8) Uwe makini na mawazo yanayokujia mara baada ya kuwa umeota (umeamka),yanaweza pia yakawa yanazungumza kitu kuhusiana na ndoto uliyoota.

ANGALIZO:-

Neno la Mungu na Roho Mtakatifu ndio msingi mkubwa wa Mungu kuzungumza na watu wake katika zama hizi za agano jipya, KWA HIYO ILI KUZIELEWA NDOTO NA KUCHUKUA MAAMUZI SAHIHI NI MUHIMU SANA SANA MTU AWE AMEJAZA NENO LA MUNGU NDANI YAKE NA KUMTEGEMEA ROHO MTAKATIFU KWA KUMPATIA TAFSIRI SAHIHI NA MAELEKEZO YA NINI CHA KUFANYA. Bila Msingi mzuri wa Neno la Mungu na mahusiano mazuri na Roho Mtakatifu, shetani pia anaweza kutumia ndoto na kumvuruga mtu na hata kusababisha mafarakano kabisa. 

USHAURI:-

Mwl. Christopher Mwakasege ameandika vitabu viwili vya ndoto (NDOTO - 1&2) na humo ameeleza maana ya ndoto nyingi na namna ya kuziombea au hatua sahihi za kuchukua. Ninashauri kwa ambaye anapenda kujifunza zaidi atafute vitabu hivyo. 

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

#Umebarikiwa

~Na. Mwl Francis M Langula

+255754711247

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!