Text

Sauti ya Mungu Kwenye Wazo la Kawaida

1 views 1 day ago

2 Wafalme 7:3-4 “Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.
Najaribu kuwaza kama hawa wakoma wangepuuzia wazo (idea) jema lililokuja ndani yao la KULIENDEA JESHI LA WASHAMI. 
Huu mjadala au wazo la kuwaendea jeshi la washami lilikuja kama wazo la kawaida kabisa na wala halikuwa na hata dalili yoyote kama ni sauti ya Mungu kwa hawa wakoma na yenye msaada kwa Taifa zima. 
Inawezekana mmoja wao alilileta na wakaanza kulijadili, kilichosukuma (trigger) wazo ndani yao inawezekana ni ile hali ya kuona wamefika mwisho kabisa wa uwezo wao na kinachofuata ni kufa.
Yaani, tunaona kifo mbele yetu, hatuoni njia, tunaona giza na wakati huo likaja wazo la kutokubali kukaa tu na kusubiri kifo. Wakalijadili na wakaamua wafe wakati wanafanyia kazi wazo fulani zuri ndani yao kuliko kufa wakiwa wamekaa. 
Sasa huwezi jua walishajaribu mambo mangapi hayatokei lakini walipopata wazo jema hawakulipuuzia. 
Sasa turudi nyuma kidogo, unajua kabla ya hili wazo kulikuwa na tamko la Mtumishi wa Mungu, Nabii Elisha?
2 Wafalme 7:1 Elisha akasema, Lisikieni neno la BWANA; BWANA asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.
Siku moja kabla ya tukio hili la hawa Wakoma wanne, Nabii Elisha alitoa tamko kwamba Kesho chakula kitapatikana kwa bei nafuu kabisa. 
Kumbuka kulikuwa na njaa nzito sana katika mji sababu mji wote ulikuwa umezungukwa na Maadui (Washami) kwa hiyo hakukuwa na chakula kinaingia ndani ya mji mpaka chakula kilichokuwa ndani ya mji kikaisha kabisa. 
Njaa ilikuwa kali kiwango ambacho mavi ya njiwa yalikuwa yanauzwa, ikazidi mpaka wamama wawili wakapatana kula watoto wao na wakamla mmoja. 
2 Wafalme 6:25, 28 -29 Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake.
Baada ya njaa ya kiwango hicho, ndipo nabii Elisha akasema "Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli" 
Na baada ya tamko hilo la Elisha, kesho yake alfajiri ndipo sasa WAZO HILO LA KUWAENDEA WASHAMI linakuja kwa hawa wakoma wanne, wao wakiwa hawajui chochote kinachoendelea ndani ya mji wala kuhusu tamko la Nabii Elisha. 
Wao walichokuwa wanakifikiria ni njaa yao binafsi, hawakuwa wanafikiria TAIFA ZIMA, lakini wazo walilokuwa wanalijadili lilikuwa ni la KITAIFA. 
Yaani, Mungu anawaletea wazo la KUOKOA TAIFA wao wanalijadili kama wazo la kifamilia au la kikundi. 
Unajua Mungu ni mkuu, na mawazo yake yako juu mno, sio madogo madogo japo wazo lake linapomjia mtu laweza kuja kwa njia ya kawaida kiasi ambacho anaweza alipuuze hasa akijilinganisha hali yake ya nje na namna wazo lilivyo. 
Najaribu kuwaza wangelidharau hili wazo na wasingelichukulia hatua, WANGEDHANI WAMESABABISHA MADHARA KWAO PEKE YAO, LAKINI UKWELI NI KWAMBA WANGESABABISHA MADHARA KWA MAELFU NA VIFO VINGI SANA. 
Mara ngapi TUMEPUUZIA WAZO ZURI LA MUNGU, kwa sababu za kibinafsi, ambalo tungelifanyia kazi LINGEOKOA MAELFU? 
How many times we ignored GOOD IDEA FROM GOD which would have saved the multitude?
Neno la Mungu linasema Mungu anatuwazia mawazo mema, ya amani na kutufanikisha. 
Yeremia 29:11Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
Ni kweli Mungu anatuwazia mawazo mema, lakini, ili mawazo hayo yawe halisi kwetu huwa anayaleta kwetu au kwa mtu (inaweza kuwa mtu binafsi, au taasisi au serikali) ayatekeleze na kuyafanyia kazi. 
Yakibaki kwa Mungu bila kudakwa huku duniani na kufanyiwa kazi yatabaki kuwa mazuri lakini sisi hatutayafaidi uhalisia wake. 
Isaya 55: 8-11  Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.
Hayo mawazo ya Mungu na njia za Mungu ni lazima zifunuliwe kwetu ili yawe halisi tufurahie. 
Ndio maana Daudi akasema Zaburi 25:4 Ee BWANA, unijulishe njia zako, Unifundishe mapito yako,
Mithali 23:26 Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.
Zaburi 103:7 Alimjulisha Musa njia zake, Wana wa Israeli matendo yake.
Inawezekana kabisa tukayajua mawazo ya Mungu na kuzijua hizo njia za Mungu ambazo ziko juu sana. Njia za Mungu zinaweza kutafsiriwa kama MBINU ZA MUNGU kutufikisha alipokusudia au kutufanikisha. 
Lakini pia ukiunganisha msitari wa 8, 9 na 11 kwenye Maandiko hayo niliyonukuhu kutoka kwenye kitabu cha Isaya 55 utagundua Neno la Mungu ni Mbegu yenye wazo la (maelekezo ya) Mungu ndani yake, likifanyiwa kazi litafanikiwa na kutimiza makusudi ya Mungu. 

Neno la Mungu katika kinywa cha Nabii Elisha kwamba, "kesho chakula kitapatikana tele" (2 Wafalme 7:1) lilikuwa ni mbegu ambayo ndani yake ilikuwa na WAZO LA MUNGU, ambalo (hilo wazo) lilidondoka mioyoni mwa WAKOMA (Watu wasiotegemewa kabisa) WANNE, na walipolifanyia kazi, ile mbegu ikafanikiwa na chakula kikawa tele siku ya pili sawa sawa na Neno la Mungu kupitia Nabii Elisha. 
Wakati mwingine Mungu hudondosha mawazo yake (au wazo lake) ndani yetu kwa namna ya kawaida sana, na tusipokuwa makini tunaweza kujikuta tunapishana na miujiza yetu na kuwakosesha wengi majibu yao kwa sababu tu ya kupuuzia ukawaida wa wazo la Mungu. 
Hawa wakoma siku zote walikuwa pale lakini hawakuwahi kuwaza hivi, kwa hiyo wazo hili jema hawakupaswa kulipuuzia kabisa. 
Umekaa kwenye hali fulani muda mrefu na ni kama ulikuwa umeamua kuanza kuridhika nayo na ghafla linakuja wazo la kuchukua hatua au kufanya jambo, uwe makini na wazo hilo. 
Kinachoniogopesha katika mfano huu ni kwamba, hakuna dalili yoyote iliyoonyesha kwamba HILI WAZO NI SAUTI YA MUNGU NA LIMEBEBA MAJIBU, hicho ndio kinanifanya niwaze ni mara ngapi nimepuuzia mawazo ya Mungu? 
Kuanzia leo, UNAPOPATA WAZO JEMA, ni vizuri kwanza kulikubali hata kama unaona limekuzidi au halitekelezeki kirahisi; likubali kwanza, ikiwezekana liandike kabisa, kisha anza kuliombea, yaani lipeleke mbele za Mungu, na kwa kadiri unavyoliombea, kama limetoka kwa Mungu utazidi kuwa na amani nalo lakini pia Mungu ataanza kukufunulia hatua (njia) ndogo ndogo za utekelezaji na baada ya hapo, chukua hatua, anza kulifanyia kazi linaweza kuwa limebeba MUUJIZA WAKO NA WA WATU WENGI NYUMA YAKO. 
 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa

~Na Mwl. Francis M. Langula

+255754711247

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!