Text

SIKU ZOTE NI MAPENZI YA MUNGU KUPONYA

2 views 1 day ago

LK. 14:1-6

1 Ikawa alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. 2Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. 3Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo? 4Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake. 5Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? 6Nao hawakuweza kujibu maneno haya.

MAMBO YA KUJIFUNZA:

LK 14:1 Ikawa alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia.2Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura. 3Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo? 4Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake.

- Yesu hakuingia kwenye nyumba ya huyu mkuu wa mafarisayo kwa ajili ya kuponya, bali aliingia ili ALE CHAKULA.

- Lakini alipomuona tu mtu ana UGONJWA wa safura [Ugonjwa wa kuvimba mwili], alipata shida kumuona katika hali hiyo na akatamani kufanya kitu.

- Inaonekana, mazingira hayakuwa rafiki sana kuponya kwa sababu aliokuwa nao ni wapinzani wa uponyaji hasa siku ya sabato.

- Lakini mazingira hayakuwa kizuizi  cha Yesu kumponya yule mgonjwa.

- YESU bila kuulizwa na mtu wala kuombwa na mtu, AKAMSHIKA, AKAMPONYA MGONJWA.

Hiki YESU alichofanya kinadhihirisha MAPENZI YA YESU KUPONYA YA HALI YA JUU SANA kwa sababu zifuatazo:-

  1. Alikwenda pale kwa ajili ya mualiko wa chakula na si kuponya      lakini aliponya.       
  2. Mgonjwa huyu hakumuomba YESU amponye, lakini *aliamua kumponya. *
  3. Hatuna uhakika kama kweli mgonjwa alikuwa na imani yoyote ya kuponywa, lakini aliponywa.
  4. Mazingira aliyokuwa nayo YESU hayakuwa rafiki kuponya, maana alikuwa amezungukwa na wakuu ambao hawakukubaliana na uponyaji siku ya sabato lakini aliponya siku ya sabato.
  5. Kwa kuponya siku ya sabato, Yesu alihatarisha maisha yake, kwa sababu ilikuwa mtu anayevunja sabato anastahili kuuawa, lakini hakujali hilo bado alimponya.

YESU ANATAMANI KUKUPONYA KULIKO WEWE UNAVYOTAMANI KUPONA.

LK 14:5 Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng’ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato? 6Nao hawakuweza kujibu maneno haya.

- Yesu anamuona kila anayeteswa na magonjwa, ni sawa kabisa na punda au ng'ombe aliyetumbukia kisimani mbele ya macho ya mwenye mnyama huyo; hii haimaanishi Yesu anatuona kama wanyama, lakini inamaana kuwa kama vile mtu asivyoweza kumuacha mnyama wake ateseke eti kwa sababu ya sheria za dini, ndivyo ilivyo kwa YESU, ANATAMANI KUMUONA KILA ALIYE KATIKA KIFUNGO CHA MAGONJWA AKIPONA KABISA.

USIWE NA SHAKA JUU YA KUSUDI LA MUNGU KUKUPONYA, NI KUSUDI LAKE KUKUPONYA KABISA SASA HIVI.

MUNGU      ASINGERUHUSU MWANAE APIGWE  KWA SABABU YETU WAKATI HANA UHAKIKA KAMA KWELI NI MAPENZI YAKE ATUPONYE..... Maana, "Kwa kupigwa kwake Yesu tuliponywa" 

Hata unaposoma ujumbe huu, unaweza ukaamini na kuchukua uponyaji wako kwa chochote kinachokusumbua! 

Unapoamini tu, tayari umetengeneza mazingira ya kupokea uponyaji hata kama hauko kanisani! Kwa sababu SIKU ZOTE NI MAPENZI YA YESU KUPONYA

Sijali ni ugonjwa gani unaumwa, usiogopeshwe na majina mbali mbali ya magonjwa, ninachojua SIKU ZOTE NI MAPENZI YA YESU       KUPONYA, Hata sasa yuko tayari kuponya. 

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!