Text

Tumia Fikira Zako Kwa Usahihi Zikupatie Ushindi

1 views 1 day ago

Wakolosai 3:1-3 SUV

“Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.”

Neno hilo nililonukuu hapo juu linaweka wazi kitu cha muhimu sana sana.

Basi kwa kuwa tumefufuliwa pamoja na Kristo, sehemu ya kwanza inasema tunapaswa kuyatafuta yaliyo juu na sehemu ya pili inasema TUYAFIKIRI YALIYO JUU.

Neno la Mungu linaweka wazi kwamba, kufufuliwa kwetu pamoja na Kristo ni jambo lisilopingika na limekamilika tayari, lakini linaweka MADAI MUHIMU SANA KWETU, kwamba ili tuweze kufurahia kila kilichofanyika [Kufufuliwa pamoja na Kristo] NI MUHIMU SANA TUBADILI JINSI TUNAVYOFIKIRIA.

Labda swali muhimu ni hili:- JE WEWE UNAJIFIKIRIAJE?

Unajifikiria sawa sawa na unayoona yanakuzunguka na kukutokea?

Unajifikiria kuwa WEWE NI KIUMBE MDHAIFU TU USIYEFAA KWA LOLOTE?

Unajifikiria wewe ni MWENYE DHAMBI TU?

Kuna wengine wanajifikiria WAO NI MAREHEMU WATARAJIWA TU, kwa hiyo kila mahali anaona KIFO... akipanda gari anafikiria ajali tu, akipanda bodaboda anaona ajali tu... akilala usiku anaona wachawi wakimmaliza tu... yaani yeye anajifikiria hivyo tu...

NENO LA MUNGU LINASEMA WAZI, IKIWA TUMEFUFULIWA PAMOJA NA KRISTO, LAZIMA TUGEUZE NAMNA TUNAVYOFIKIRIA... LINASEMA TUYAFIKIRI YALIYO JUU KRISTO ALIKO...

SASA HUKO JUU HAKUNA UCHAWI, HUKO JUU HAKUNA KUSHINDWA, HUKO JUU HAKUNA AJALI, HUKO JUU HAKUNA MAGONJWA...

Sasa sio kwamba Mungu hajui mambo yanayoendelea huku duniani ikiwa ni pamoja na hatari nyingi na mashambulizi yanayotuzunguka; lakini anatuelekeza namna sahihi ya KUFIKIRI ili iwe rahisi kushinda haya yanayotuzunguka.

KILICHOMZAMISHA PETRO WAKATI AMEITWA NA YESU ATOKE KWENYE BOTI NA KUTEMBEA JUU YA MAJI, SIO MAWIMBI BALI NI PALE ALIPOACHA KUMFIKIRIA YESU NA NENO ALILOMUAMBIA "NJOO" NA AKAANZA KUUANGALIA UPEPO NA MAWIMBI.

Hata katika changamoto, ni muhimu sana kuwa na FIKIRA SAHIHI AMBAZO ZITAZALISHA MTAZAMO SAHIHI.

Neno la Mungu linasema, katika changamoto ya kuumwa na nyoka kwa wana wa Israel, kilichowaokoa sio kwamba nyoka waliisha, bali kilichowaokoa ni KUTOA MACHO YAO KWENYE KILE KILICHOWAUMA [NYOKA] NA KUELEKEZA MACHO YAO [NA MAWAZO YAO] KWENYE NYOKA WA SHABA [JIBU LA MUNGU]

Mara nyingi, tunachohitaji cha kwanza SIO CHANGAMOTO KUONDOLEWA, BALI KUWA NA MTAZAMO SAHIHI SAWA SAWA NA NENO LA MUNGU HATA KATIKATI YA CHANGAMOTO; NA MTAZAMO HUU UTAZALISHWA NA KUFIKIRI KWA USAHIHI SAWA NA NENO LA MUNGU.

Neno la Mungu linasema, AONAVYO [AU AFIKIRIVYO] MTU NAFSINI MWAKE NDIVYO ALIVYO.

KWA HIYO, KUFIKIRI KUNAWEZA KABISA KUAMUA MATOKEO YA NJE YA MTU.

“Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo,.... Yafikirini yaliyo juu,.... Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” Wakolosai 3:1-3 SUV

Anza kujifikiria kama Mungu anavyokufikiria. ANZA KUUONA UHAI WAKO UMEFICHWA PAMOJA NA KRISTO KATIKA MUNGU. Ukijiona na kujifikiria hivyo; hauwezi kukosa usingizi eti kwa sababu kuna mchawi anataka kukuroga.

Utagundua hawezi kukupata, kwa sababu UHAI WAKO UMEFICHWA PAMOJA NA KRISTO KATIKA MUNGU.

KUNA KITU AMBACHO WENGI HATUFAHAMU NI KWAMBA, SHETANI AKIFANIKIWA KUKUFIKIRISHA KINYUME NA NENO LA MUNGU [ELIMU YA MUNGU] JUU YA JAMBO LOLOTE UNALOLIPITIA, BASI AMEFANIKIWA KUKUPATA.

"Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;" 2 Wakorintho 10:3-5

SHETANI HACHUKULII FIKIRA NA MAWAZO YETU KAMA KITU CHA KAWAIDA KWA JINSI AMBAVYO SISI TUNAONA, YEYE ANAJUA HUO NI UWANJA WA VITA, NA AKIPATA FIKIRA AMEMPATA MTU.

KWENYE FIKIRA, NDIPO ADUI HUJENGA NGOME YAKE

Kwa hiyo, kwenye kila eneo la maisha yako, HAKIKISHA UNAFIKIRI SAWA SAWA NA NENO LA MUNGU.

Kila wazo linalopingana na Neno La Mungu linapoinuka, hakikisha unalizima na unawaza sawa na ELIMU YA MUNGU. kwa jinsi hiyo, utakuwa unasababisha ushindi kwenye vita yako ya kiroho.

Hata wakati anataka kumuangusha Hawa, alihakikisha anamfikirisha Hawa tofauti na Neno la Mungu au Agizo la Mungu. Shetani alipindisha kidogo tu maagizo kwenye fikira za Hawa na ndipo akampata.

"Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo." 2 Wakorintho11:3 (SUV)

Hata wanaomkataa Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yao, ni kwamba SHETANI amepofusha fikira zao

"ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu." 2 Wakorintho 4:4 (SUV)

NENO LA MUNGU LINASEMA WAZI KWAMBA, KUFIKIRI NA KUOMBA KUNAWEZA KUFANYA KAZI SAWASAWA KABISA.

"Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;" Waefeso 3:20

ANDIKO LETU KUU LINASEMA HIVI:- 

“Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” Wakolosai 3:1-3 SUV

Kwa hiyo, anza kujifikiria sawa sawa, anaza kufikiria sawa sawa. KUYAFIKIRI YALIYO JUU NI KUFIKIRI SAWA NA NENO LA MUNGU!

NINAAMINI KWA KUFANYA HIVYO, TUTAANZA KUONA MABADILIKO MAKUBWA KWENYE IMANI ZETU NA BAADAYE TUTAANZA KUONA MATOKEO KWENYE KILA ENEO LA MAISHA YETU

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

Umebarikiwa

~Na. Mwl. Francis M. Langula

(+255754711247)

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!