Udanganyifu wa Moyo na Namna ya Kuushinda
Yeremia 17:9-10
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua? Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.
Kuna mambo mawili ya kutisha yamehusishwa na moyo wa mtu.
Moja, ni udanganyifu kuliko vitu vyote na mbili, ni ugonjwa wa kufisha au wa kuuwa.
Neno linaposema udanganyifu kuliko vitu vyote, inamaana kama tukipima viwango vya udanganyifu wa watu na vitu, basi udanganyifu wa moyo wa mtu uko kiwango cha juu zaidi.
Sijui kama umeshawahi kukutana na watu wanaojua kudanganya... Lakini pia kuna vitu vinajua kumdanganya mtu mpaka akajisahau, ikiwemo pesa, afya, mali na vingine vingi... Lakini Neno linasema Moyo umezidi vyote.
Tunajua kiwango cha juu au mafanikio ya udanganyifu ni pale unapoweza kudanganywa bila wewe kugundua mpaka mwisho kabisa au mpaka it's too late.
Sasa moyo ndio una viwango hivyo vya udanganyifu, yaani moyo wa mtu unaweza ukawa unamdanganya mtu bila mtu mwenyewe kugundua, na unaweza ukafanya hivyo mpaka huyo mtu akafa kabisa kiroho, au kimwili au vyote viwili na akajikuta yuko jehanam (too late).
Moyo unaweza kutumia DHAMBI, KIBURI, MAFANIKIO, TAMAA, PESA nk katika kumdanganya mtu...
Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?
Maandiko hayo pia yanasema, huo huo moyo ambao ni mdanganyifu, una ugonjwa unaoitwa UGONJWA WA KUFISHA... Au kwa lugha nyingine, Moyo unaumwa ugonjwa wa kuua.
Halafu Neno la Mungu linauliza, ni nani awezaye kuujua?
Ninaamini hapo ndipo ilipo shida kubwa zaidi, kuumwa ni tatizo, kuumwa halafu hujui unaumwa nini ni tatizo kubwa zaidi. Na hilo ndio tatizo kubwa la moyo, UNAWEZA UKAMDANGANYA MTU na muhusika asijue kabisa kama moyo wake unamdanganya.
Mungu amesema yeye ndio mtaalam (expert) wa kuichunguza mioyo yetu... Anaijua vizuri san a.
Lakini Mungu ni mstaarabu sana, pamoja na kwamba anaichunguza na kuijua mioyo yetu, hatafanya chochote mpaka tumkabidhi hiyo mioyo, kama hatutamkabidhi, inaweza kuendelea kutudanganya na Mungu yupo anaijua.
Ndio maana Neno linasema "Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu. "
Mithali 23:26
Mungu anauomba moyo wako na wangu, tukimkabidhi ndipo sasa, atatufungua macho yetu, tuone kama kuna chochote hakiko sawa kwenye mioyo yetu na tukishughulikie.
Zingatia: 1 Ni vizuri kujijengea tabia ya kuombea moyo wako, kumwambia Mungu ninakukabidhi moyo wangu na kumwambia pia unichunguze m oyo wangu, na unijulishe kama kuna udanganyifu wowote lakini pia uniumbie moyo safi.
Kudhihirisha ninachokizungumza kuhusu m oyo na umuhimu wa kuombea moyo, naomba ninuku u maneno ya Daudi akiuombea moyo wake, kutoka katika kitabu cha Zaburi 51:10 "Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya na kuithibiti roho yangu."
Labda kwa kukukumbusha tu, maneno hayo ya Zaburi 51, Daudi aliyazungumza baada ya kuigundua dhambi yake, baada ya kukutana na Nabii Nathani kama ilivyoandikwa katika 2Samuel 12.
Moyo wa mtumishi wa Mungu Daudi ulimdanganya, akalala na mke wa Uria (na hakugundua dhambi yake) , ukaendelea kumdanganya akamuua Uria vitani (bado hakuigundua dhambi yake), bado mpaka amekutana na Nabii Nathani hakugundua, mpaka anatolewa mfano wa Kondoo na Nabii bado haelewi, mpaka anatoa hukumu ya kifo kwa mtu aliyefanya kosa la aina yake bado haelewi.
Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule; akamwambia Nathani, Aishivyo BWANA, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake astahili kufa;
2 Samweli 12:5
Mwisho kabisa Nabii Nathani akamwambia ukweli, kwamba huyo mtu aliyetenda hayo ni wewe.
Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo. BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nilikutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli, nikakuokoa kutoka kwa mkono wa Sauli;
Kwa nini umelidharau neno la BWANA, na kufanya yaliyo mabaya machoni pake? Umempiga Uria, Mhiti, kwa upanga, nawe umemtwaa mkewe awe mke wako, nawe umemwua huyo kwa upanga wa Waamoni.
2 Samweli 12:7,9
Ndipo Daudi anagundua kosa lake na ndipo anaomba maombi ya Zaburi 51. Na katika maombi hayo ndipo unagundua Daudi alijua wazi MOYO WAKE NDIO ULIMDANGANYA NA KUMKOSESHA, na ndipo akaamua kuanza kuji ombea Moyo wake.
Daudi anasema "Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya na kuithibiti roho yangu. "
Zaburi 51:10
Anamwambia Mungu, nimegundua huu moyo wangu ndio ulinidanganya na kunifikisha hapa na mimi sikujua kabisa, nakuomba UNIUMBIE MOYO SAFI, unipe uwezo wa kuidhibiti roho yangu... Yaani niwe na uwezo wa kugundua hapa ninavuka mpaka na niweze KUJIZUIA. Niwe na KIASI (SELF CONTROL), Niwe na uwezo wa kujidhibiti macho yangu yasiukosehe moyo, niweze kuunidhamisha moyo na kuwa na nidhamu binafsi (SELF DESCIPLINE). Eee Mungu uniumbie moyo safi.
Haya yanapaswa kuwa maombi yetu pia.
Binafsi, haya ni maombi yangu ya dhati kabisa mbele za Mungu.
Eee Mungu, uniumbie Moyo Safi. Moyo wangu usije ukanidanganya kwamba niko salama kumbe ninaangamia, uuponye moyo wangu na ugonjwa... Eee Mungu, usiuache moyo wangu kunikosesh a.... Ninakupa moyo wangu kila siku, hata leo ninakupa moyo wangu, ili siku zote, macho yangu yapendezwe na sheria zako.
Mungu ametupa wajibu wote kwa mioyo yetu, ndio maana mahali pengine anatuagiza "LINDA MOYO WAKO KULIKO YOTE UYALINDAYO..."
Mahali pengine Daudi anafunua siri nyingine aliyoitumia kuudhibiti moyo wake usimkoseshe tena.
Zingatia: 2 Anasema katika Zaburi, MOYONI MWANGU NIMELIWEKA NENO LAKO, NISIJE NIKAKUTENDA DHAMBI.
Kwa hiyo, njia nyingine nzuri ya kuutunza moyo usikudanganye, ni kulijaza Neno la Mungu Moyoni mwako.
Neno la Mungu lina uwezo wa KUYATAMBUA MAKUSUDI YA MOYO, kwa hiyo litakusaidia kuulinda moyo wako usikudanganye.
PAMOJA NA KWAMBA MOYO NI MDANGANYIFU, NIMESHAGUNDUA CHA KUFANYA... UDANGANYIFU WAKE HAUTANIPATA.
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author