Unamuhitaji Yesu, Sio Watu
Yohana 5:6-8
“Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. “
Ni mara ngapi tunapishana na miujiza yetu kwa kuwafikira na kuwategemea watu?
Huyu mgonjwa, kwenye ufahamu na moyo wake alikuwa anafikiri anahitaji watu ndipo APONYWE.
Hakuwa anajua aliyenaye ni zaidi ya mtu au watu aliokuwa anawahitaji.
Na ukifuatilia kwa makini, huyu mgonjwa hitaji lake halisi halikuwa watu, hitaji lake lilikuwa KUPONYWA.
Yeye anadhani anahitaji watu kumbe anahitaji KUWA MZIMA.
Sasa unaweza kuona kuwafikiria watu kulivyomfunga macho na moyo wake kiasi kwamba asijue hata anachohitaji sio watu bali ni kuwa mzima.
Hii inat hibitishwa na namna alivyojibu swali la Yesu.
“Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima?” Yohana 5:6
Swali la Yesu lilienda moja kwa moja kwenye HITAJI LA HUYU MGONJWA. Lakini alichojibu kinadhihirisha KUWATEGEMEA WANADAMU kulivyomgeuza moyo na ufahamu wake.
Yesu anamuuliza, WATAKA KUWA MZIMA? yeye anajibu, MIMI SINA MTU.
Na kibaya zaidi, macho yake yalipofushwa hata yasimtambue au yasitambue uwezo wa aliyemuuliza, japo wakati anamjibu alimuita BWANA.
“Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu...” Yohana 5:7
Hii ndio hali tuliyonayo watu wengi. Japo tunamuita Yesu Bwana, lakini tumepofushwa na kuwategemea wanadamu na kusahau uweza wa huyu tunayemuita BWANA.
Tunamuita BWANA lakini tunamwambia hatuna mtu wa kutusaidia.
Kikubwa kilichomuathiri huyu Mgonjwa ni historia ya eneo lile na namna ambayo watu walikuwa wakiponywa. Au kwa lugha nyingine, kilichomuathiri ni mfumo uliokuwepo.
Mfumo ndio uliokiwepo ulikuwa unaonyesha kwamba, ili apone anawahitaji watu.
Ninaamini hicho ndicho kinachotutesa wengi pia. MFUMO WA DUNIA HII UMETUATHIRI.
Mfumo unasema kwamba, ili nipate kazi mahali fulani, basi NINAHITAJI MTU WA KUNISHIKA MKONO.
Mfumo huo umetukamata kiasi kwamba, tumesahau HITAJI LA MSINGI LA KAZI, NA TUKAFIKIRI TUNAHITAJI WATU NA SIO KAZI. YAANI INATUFIKISHA HATUA HATA MUNGU AKITAKA KUTUPATIA KAZI TUNASHINDWA KUMUAMINI NA KUMWAMBIA HATUNA WATU WA KUTUSAIDIA.
Kuna wengine hadi maombi yao yamebadilika, hawaendi mbele za Mungu kumwambia Mungu NINAHITAJI KAZI, bali humwambia, LAITI NA MIMI NINGEKUWA NA MTU MAHALI FULANI NINGEPATA KAZI.
Hilo la kazi nimelisema kama mfano tu, lakini kuna mifano mingi tu.
Kuna ambao ni wagonjwa, wanahitaji uponyaji, lakini ndani yao wanawaza kwamba WANAMUHITAJI SPECIALIST au HOSPITALI FULANI na wanasema laiti ningekuwa na uwezo wa kumpata Daktari Bingwa au Hospital fulani, na wanamwambia Mungu kabisa, kwa ugonjwa huu namuhitaji Daktari Bingwa au Hospitali fulani, wanasahau wanayemueleza ni zaidi ya Daktari bingwa na anaweza kabisa kuwaponya, lakini kuwategemea wanadamu kumewapofusha macho.
Sasa sio vibaya kumuona Daktari Bingwa au kuwa na mtu wa kukusaidia au kwenda hospitali fulani.
Ninachotaka uone hapa, HATUPASWI KUWAPA WATU NAFASI YA KWANZA MAISHANI MWETU, MUNGU NDIYE ANAWEZA KUTATUA MATATIZO YETU.
Kabla ya mtu yeyote, UNAMUHITAJI YESU.
Na wakati unapofikiri HAUNA WATU, YESU YUPO HAPO HAPO KWA AJILI YA KUKUSAIDIA.
HABARI NJEMA NI KWAMBA, HATA KAMA KWELI UNAHITAJI WATU, MUNGU NDIYE MWENYE WATU SAHIHI NA NDIYE ANAYEJUA HITAJI LAKO LINAHITAJI WATU AU MTU WA AINA GANI, KWA HIYO AKIONA NI LAZIMA, YEYE NDIYE ATAKUPATIA WATU SAHIHI.
“Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.” Isaya 43:4
Ujumbe huu ukukumbushe, HAUHITAJI WATU, UNAMUHITAJI YESU, YEYE NDIYE ATAKUPATIA WATU SAHIHI KAMA NI LAZIMA.
Yesu anao uponyaji unaohitaji na sio watu, Yesu ndiye ana uwezo wa kukupa kibali hapo unapoomba kazi hata kama huna mtu anayekufahamu wa kukushika mkono.
Yesu anaweza kukushika mkono na kukupatia hiyo kazi, na kama ni lazima anaweza kukupatia yeye watu sahihi.
Yesu ndiye anaweza kukutana na mahitaji yako yote, na kama ni lazima, yeye atakuletea watu sahihi.
NINAKUHITAJI YESU, WEWE UNA UZIMA NINAOUHITAJI, WEWE UNA UTAJIRI WOTE, WEWE UNA AFYA NINAYOHI TAJI, WEWE UNA MAJIBU YANGU YOTE, WEWE PIA UNA WATU SAHIHI NINAO WAHITAJI MAISHANI MWANGU.
UNAMUHITAJI YESU KWANZA, SIO WATU.
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author