Upendo wa Mungu Haushindwi na Hali Unayopitia: Sehemu ya I
Warumi 8:37-39 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Ninayatafakari haya maneno mazito kwenye barua hii ya Mtume Paulo kwa Warumi na watu wote.
Anasema HAKUNA KITU CHOCHOTE KINAWEZA KUTUTENGA NA UPENDO WA MUNGU.
Turudi nyuma kidogo mstari wa 35 kisha tutafakari kwa pamoja.
Warumi 8:35 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?”
Kwenye mstari huu ametaja vitu ambavyo ukifuatilia ndio vinawafanya au vimewafanya watu wengi kutengwa au kujitenga na upendo wa Mungu.
Kuna watu wengi sana waliookoka ambao vitu vilivyotajwa hapo, yaani DHIKI, SHIDA, ADHA, NJAA, UCHI (AIBU), HATARI, UPANGA na vinavyofanana na hivyo vimewatenga na upendo wa Mungu na wamemuacha Mungu kabisa.
Hili Neno linanishangaza sana. Unajua wengi tukiuwaza upendo wa Mungu tunauwaza kwa upande wa kuishi mbali na dhiki, shida, njaa, uchi hatari nk yaani tukikutana na hivyo vitu, kitu cha kwanza kuwaza ni kwamba Mungu ameniacha.
Wetu wengi tukiwa kwenye dhiki, shida, changamoto nk hatuuoni upendo wa Mungu tunaanza kumlaumu Mungu na kuona hatupendi na ametuacha lakini Paulo anauliza Ni kitu gani kitatutenga na Upendo wa Mungu? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga?
Halafu baada ya mstari mmoja anaanza kujibu swali alilouliza katika msitari wa 35 anasema katika mstari wa 37
Warumi 8:37 “Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.”
Kumbe mambo hayo yakitujia sio kwa ajili ya kututenga na Mungu bali ni kutupatia ushindi wa juu kabisa yaani KUSHINDA NA ZAIDI YA KUSHINDA
Tafsiri ya KJVLite Version inasema "Nay, in all these things we are more than conquerors through him that loved us."
Yaani "katika mambo hayo yote, sisi ni zaidi ya washindi kupitia yeye aliyetupenda"
Huwezi kuwa zaidi ya mshindi kama hutashinda mambo hayo. Lakini kuna jambo la muhimu sana analiunganisha na huo ushindi. Anasema "KUPITIA AU KWA YEYE ALIYETUPENDA"
Kwa hiyo ushindi huu ni kwa sababu ya UPENDO WA MUNGU.
Kwa hiyo, ILI TUWE ZAIDI YA WASHINDI KATIKA MAMBO HAYO, NI LAZIMA TUWEZE KUUONA UPENDO WA MUNGU NDANI YA HIZO DHIKI, SHIDA NK.
Huwezi kushinda kama huoni UPENDO WA MUNGU unapokuwa katika shida na changamoto.
Mtu yeyote ambayo akikutana na shida halafu akaanza kuuonea mashaka upendo wa Mungu kwenye maisha yake, huyo mtu LAZIMA ATASHINDWA, hawezi kuwa zaidi ya mshindi, hawezi kushinda.
Ndio maana maandiko yanasema
1 Wakorintho 13:13 “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”
Upendo ndio msingi wa Imani na Tumaini. Kama ukishindwa kuona upendo wa Mungu katikati ya changamoto, utapoteza imani na mwisho utapoteza matumaini kabisa. Na kama ukianza kuuona upendo wa Mungu katikati ya dhiki yako, matumaini yatafufuka na imani itazaliwa pia.
Hatua ya kwanza ya adui kutushinda tunapopitia katika dhiki na changamoto ni kutufumba macho TUSIUONE UPENDO WA MUNGU.
Kama unapitia changamoto yoyote na umefika mahali huoni upendo wa Mungu, ujue utampoteza Mungu sababu ya hiyo dhiki.
Na ukweli ni kwamba, uwepo wa dhiki HAUONDOI UPENDO WA MUNGU, ni shetani tu ndio humfunga mtu macho asiuone upendo wa Mungu.
Upendo wa Mungu ni mkuu kuliko dhiki yako.
Neno la Mungu lina sema, Warumi 8:28 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.”
Anaposema katika mambo yote, anamaanisha hata katika dhiki, Mungu hufanya kazi na wale wanaompenda.
Uwepo wa moto wa majaribu hauondoi upendo wa Mungu kwenye maisha yetu.
Danieli 3:25 “Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.”
Unaweza kuwa katikati ya tanuru, dhiki, changamoto, mauti na upendo wa Mungu uko katikati yako.
Usije ukadhani kwa sababu uko kwenye changamoto basi upendo wa Mungu umekuacha au upo peke yako, Mtu wa Nne yuko pamoja nawe.
Isaya 43:2,5 “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza. Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;”
Mungu anaweza akawa nawe kwenye maji mengi na kwenye moto, na lengo kuu uwe mshindi na Zaidi ya mshindi.
Hapo juu nimekuhakishia kwamba kuwa katika changamoto au majaribu hakuondoi upendo wa Mungu na uwepo wake katikati yako.
Lakini, kuwa na upendo wa Mungu au uwepo wa Mungu ni jambo moja na KUWA NA UHAKIKA (KUJUA KWA HAKIKA) WA UPENDO WA MUNGU NI JAMBO LINGINE.
Mimi ninaamini KUTOKUJUA AU KUTOKUWA NA UHAKIKA WA UPENDO WA MUNGU KATIKA CHANGAMOTO NDIO TATIZO KUBWA linalosumbua wengi.
Je, una uhakika kwa kiasi gani kuhusu UPENDO NA UWEPO WA MUNGU kwenye maisha yako pindi unapokuwa katika dhiki au changamoto?
Huku kujua na kuwa na uhakika ni muhimu sana Ndio maana andiko tulilonukuhu la Warumi 8:28 linaanza kaa kusema "Nasi twajua..."
Lakini pia kina Shedrak, Meshak na Abednego walikuwa wanajua kuhusu Mungu wao anawapenda na anaweza kabisa kuwaokoa na yuko pamoja nao katika maamuzi hayo ya kuingia katika moto.
Lakini pia andiko nililonukuu juu mwanzoni, msitari wa 38 unaanza hivi
Warumi 8:38 "Kwa maana nimekwisha kujua hakika..."
Kwa hiyo siri ipo hapo kwenye KUJUA KWA HAKIKA kuhusu upendo wa Mungu katika maisha yako hata unapopita katika dhiki.
Kuna watu, kila changamoto wanayopitia, upendo wa Mungu kwao uko hatarini (God's love for them is at risk), na hii sio kwa sababu upendo wa Mungu hauko pamoja nao bali ni kwa sababu HAWAJUI KWA HAKIKA kuhusu upendo wa Mungu kwao.
Kuna watu kila wakipita mahali pagumu utawasikia wanasema au Mungu ameniacha? Au nimemkosea Mungu ananiadhibu? Au Mungu hanipendi? Na mengine mengi.... Ukweli ni kwamba shida kubwa ni kwamba HAWANA UHAKIKA au HAWAJUI KWA HAKIKA UPENDO WA MUNGU, na hii ni chanzo kikubwa sana cha kushindwa katika changamoto.
Warumi 8:38-39 “Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
Maandiko yanayofuata, (nililonukuu hapo juu) yanaendelea kutoa ufafanuzi wa nguvu hii ya kujua upendo Mungu kwamba haishindwi na chochote.
Kimsingi anataja shida ngumu zaidi lakini anataja na hali nzuri pia.
Anataja mauti, uzima, malaika, mamlaka, yaliyopo na mengine yote. Yaani ametaja kila unachokijua.
Unajua kuna watu mauti imewatenga na upendo wa Mungu, lakini pia kuna watu uzima, afya na mafanikio vimewafanya wakawa na kiburi na kuwatenga na upendo wa Mungu.
Kuna umuhimu wa kuuona upendo wa Mungu kwenye kila hali tunayopotia. Ni hatari sana kutouona upendo wa Mungu kwenye tunayopitia.
Ukipita kwenye changamoto uuone upendo wa Mungu, lakini pia ukipita kwenye maisha mazuri uuone upendo wa Mungu.
Ukifanikiwa kuuona upendo wa Mungu katika kila hali (Nzuri na Mbaya) HAKUNA CHOCHOTE KINACHOWEZA KUKUTENGA NA UPENDO WA MUNGU, NA HAKUNA CHOCHOTE KINACHOWEZA KUKUZUIA KUWA ZAIDI YA MSHINDI.
Upendo wa Mungu haushindwi na chochote.
1 Wakorintho 13:8 “Upendo haupungui neno wakati wo wote;”
Andiko hilo kwenye Tafsiri ya ISV inasema hivi "Love never fails" yaani UPENDO HUWA HAUSHINDWI.
Ukiona kushindwa ujue KUNA SIRI YA UPENDO HAIJAGUNDULIKA.
Tutaendelea tena na sehemu ya pili ya tafakari hii ambapo nitajibu maswali Yafuatayo:-
Nifanye nini ili niweze kuuona upendo wa Mungu katika hali zote?
Mbona kuna wakati najikuta tu nikipita katika dhiki nashindwa kuuona upendo wa Mungu?
Najikuta kama upendo wa Mungu ninaouona UNAZIDIWA NA DHIKI NINAYOPITIA?
Waefeso 3:16-19 “awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.”
Waefeso 1:17-18 “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;”
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa
~Na Mwl. Francis M. Langula
+255754711247
Mwl. Francis Langula
Author