Text

Usichokuwa Nacho Hakikusaidii, Usihangaike Nacho, Badala yake Kiendeleze Ulichonacho.

1 views 1 day ago

Matendo ya Mitume 3:6

“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.”

Kwenye andiko hilo nililonukuhu, Petro na Yohana wakiwa wanaingia hekaluni kusali, wakakutana na mtu mwenye uhitaji.

Mtu huyu alifikiri anahitaji fedha au dhahabu lakini hitaji lake la kweli halikuwa fedha wala dhahabu bali uzima.

Kuna watu wengi wanafikiri wanachohitaji ni fedha au dhahabu, lakini ukweli ni kwamba wanahitaji kitu kikubwa zaidi ya fedha na dhahabu, WANAHITAJI UZIMA, WANAMUHITAJI YESU...

Lakini hicho sicho ambacho ninataka kukizungumzia kweye ujumbe huu. Kwenye tafakari hii, nataka tuangalie upande wa Petro na Yohana...

Petro anasema "Mimi sina fedha, wala dhahabu"...

Kwa hiyo Petro alikuwa anatambua ASICHONACHO...

Kutambua usichonacho (ambacho huna) si kitu cha ajabu sana japo jambo hili lilikuwa ni moja ya tatizo la yule kiwete... Kiwete alitambua asichonacho lakini si kwa ukamilifu wake, sababu hakuwa na fedha lakini kubwa zaidi hakuwa na uzima.

Watu wengi, kama vile tu Petro, ni rahisi kutambua ambavyo hatuna, japo, kama vile yule kiwete inawezekana tusitambue chanzo cha kutokuwa na hivyo tusivyokuwa navyo kwa hiyo hata hiyo kutambua tusichonacho si kwa ukanilifu wake...

Sasa turudi kwa Petro....

Petro alitambua kuwa HANA FEDHA WALA DHAHABU...

Kujua usichonacho ni hatua ya kwanza au kwa lugha nyingine kujua mahali kuna tatizo ni hatua ya kwanza...

Petro alijua Kiwete ana tatizo, ANAHITAJI FEDHA NA DHAHABU, lakini pia alijua hali yake halisi ya nje kutokana na tatizo hilo kwamba HANA FEDHA WALA DHAHABU...

Ninaamini watu wengi tungeweza kuishia kwenye hiyo hatua ya kwanza... Ya kujua tatizo kwa nje, na kujua uhalisia wako wa nje, kwamba huna uwezo wa nje wa kulitatua...

Lakini, kuna jambo muhimu sana la KUJIFUNZA KWA PETRO...

Naamini Petro alitambua siri inayopatikana kwenye kitabu cha 2 Wakorintho 8:12 "Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo."

Ya kwamba kibali cha (kukubaliwa kwa) mtu hakipatikani kwa ASIVYO NAVYO BALI ALIVYO NAVYO...

Petro akaamua asikwamie kwenye kutokuwa na FEDHA WALA DHAHABU ambapo watu wengi tumekwamia hapo.

Wengi tunaangalia sana tusivyokuwa navyo na tunakwamia kwenye tusivyokuwa navyo.

Utasikia mtu anasena unajua mimi ni masikini, mimi sina kitu kabisa, mimi ni mgonjwa, mimi ni mdhaifu, mimi nimepungukiwa na kadhalika na kadhalika...

Petro hakuwa amekamilika, hakuwa na fedha hakuwa na dhahabu, kwa lugha ya sasa hakuwa na pesa (he was broke) lakini hakukwamia kwenye kutokuwa na fedha na dhahabu.

Petro alitambua na UPANDE WAKE WA PILI AKASEMA "lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende."

Hakunaga mtu ambaye HANA UPANDE WA PILI...

Hata mtu ambaye hana kitu, upande wa pili ANACHO KITU...

Petro akagundua, pamoja na kwamba sina fedha wala dhahabu, lakini MIMI SIKO EMPTY, MIMI SIO DEBE TU, ndani yangu NINAO UZIMA.

Petro akatambua, KITAKACHONIPA KIBALI AU KUKUBALIKA, SIO KUENDELEA KUZUNGUMZIA AMBACHO SINA BALI NI KUANZA KUDHIHIRISHA AMBACHO UNACHO...

Kuna watu wanafikiri kwa kuendelea kusisitiza wao ni masikini hawana kitu cha kuchangia (simaanishi pesa pekee) kwenye jamii, hawana kitu cha kutoa (they have nothing to offer or to contribute) ndio wataonewa huruma na kupata chochote... Mawazo hayo ni kinyume kabisa na utendaji wa kanuni za ufalme wa Mungu.

Kanuni ya ufalme inasema, kama huna kitu usitegemee kabisa kupokea chochote, na kimsingi tegemea kupoteza hata kidogo ulicho nacho...

Usichokuwa nacho hakiwezi kukusaidia kwa hiyo haina maana kuendelea kusisitiza upande wako wa udhaifu au kupungukiwa, badala yake ni vizuri kuanza kutazama upande wako wa pili...

Mathayo 25:29 “Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

Mithali 11:24 “Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi;Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.”

Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

Maandiko hayo yanathibitisha kanuni hii ya KUTAMBUA ULICHO NACHO...

Kwa hiyo kila anaye focus kwenye ambacho hana hawezi kwenda mbali kwenye eneo lolote la maisha.

Jaribu kufikiria MWANAFUNZI masaa yote anajifikiria mimi sina akili kabisa darasani, huyu HAWEZI KUFAULU HATA SIKU MOJA... Lakini Mwanafunzi huyo huyo akaanza kuwaza masaa yote kwamba mimi nina uwezo mkubwa sana na lazima nitafaulu, mtazamo huo utamfanya apate mbinu za kusoma mpaka mwisho wa siku atafaulu kwa hakika.

Kuna watu wameokoka na wana Roho Mtakatifu ndani yao na wana nguvu za Mungu ndani yao lakini, KWA KUTOKUIJUA KANUNI HII, NGUVU ZA MUNGU NDANI YAO HAZIWASAIDII.

Mtu ana Yesu, lakini masaa yote anawaza maadui zake tu, anawaza wachawi, anawaza kurogwa, anawaza biashara au kazi yake imerogwa, anawaza magonjwa yatampata na kummaliza na hawazi kabisa yule aliye naye.

Kila linapokuja jambo ambalo huna, kumbuka kuna upande wa pili wa ULICHO NACHO... ukikaza mawazo yako (uki-concentrate) kwenye ambacho huna utakikuza zaidi mbele yako kiasi ambacho ULICHO NACHO HAKITAKUWA NA NGUVU YA KUKUSAIDIA...

Tuangalie maandiko mengine yanayoweka wazi kanuni hii muhimu sana.

1 Wafalme 17:12,15-16 “Naye akasema, Kama BWANA, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa kinywa cha Eliya.”

Ashukuriwe Mungu, huyu mwanamke mjane HAKUISHIA KUSEMA SINA KITU... aliendelea hatua ya pili AKAONA ANACHO KITU...

Luka 9:13 “Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula.”

Wanafunzi wa Yesu pia hawakuishia KUONA WASICHOKUWA NACHO, bali waliona zaidi ya hapo, waliona MIKATE MITANO NA SAMAKI WAWILI.

Ukilinganisha idadi ya watu na hiyo mikate mitano na samaki wawili, hakukuwa na maana kabisa kutaja walicho nacho, lakini Mungu alitumia hicho hicho ambacho kilikuwa hakina uwiano na idadi ya watu na akawalisha maelfu ya watu.

Swali muhimu sio HAUNA NINI bali ni UNA NINI?

Acha kupambana na usivyonavyo, angalia namna gani ulichonacho kitakufaa kwa sababu, "mtu hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo, si kwa kadiri ya asivyo navyo"

Kuna watu wamekwamishwa na watu ambao wameshawapoteza. Mtu ameondoka maishani kwako miaka imepita lakini bado nafsi yako imenaswa na mtu usiyekuwa naye kiasi cha kutoona watu ulionao. Hii haijakaa sawa, ondoa macho yako kwa aliyekuacha, hana msaada tena kwako.

Kutoka 4:2-4 “BWANA akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake. BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako, kamshike mkia; (akaunyosha mkono wake akamshika, naye akageuka kuwa fimbo mkononi mwake;)”

Mungu hakumuuliza Musa "NI NINI AMBACHO HUNA MKONONI?" bali alimuuliza "NI NINI HICHO ULICHONACHO MKONONI MWAKO?" na kupitia alicho nacho Musa, Mungu akafanya muujiza.

Niliwahi kukutana na kijana wa miaka 23 amekata tamaa kabisa ya kuishi sababu tu hana kitu yaani hana pesa, wakati ni mzima wa afya ana nguvu zote na akili timamu, hii ni hatari sana, baada ya kuongea naye kwa muda na kuomba naye aligundua alikuwa anaangalia upande usio sahihi...

Mtu ambaye anaangalia asichokuwa nacho muda wote hufikiria kupewa na hata siku moja hafikirii kutoa. Haoni cha kutoa sababu anaangalia upande mbaya. Mtu wa aina hii hata akipewa leo kesho atataka apewe tena kwa sababu anachoangalia ndio kinamfanya kuwa tegemezi.

Umeshawahi kuona mtu ameshakuwa mtu mzima lakini bado analaumu waliomlea (wazazi au walezi) kwamba hawakumuwezesha. Analaumu wazazi, huyu mtu ameangalia asivyo navyo na si ajabu hawezi kwenda mbali.

Inawezekana ni kweli kabisa kuna jambo hawakukufanyia sawa, lakini HILO AMBALO HUNA HALITAKUSAIDIA UKIENDELEA KULING'ANG'ANIA... Toa macho yako hapo anza kuangalia upande wa pili, angalia nguvu alizokupa Mungu, angalia VIPAWA ULIVYONAVYO, angalia FURSA unazoziacha kila siku sababu hujazitazama kwa umakini, angalia watu sahihi Mungu anaokuunganisha nao ambao kuna mahali mnaweza kupiga nao hatua kutoka hapo.

Matendo ya Mitume 3:6 “Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.”

Ukisoma vizuri andiko hilo utagundua, UHAKIKA ALIOKUWA NAO PETRO KWAMBA HANA KITU (FEDHA NA DHAHABU) NDIO UHAKIKA HUOHUO ALIKUWA NAO KWAMBA ANAO UZIMA WA KUMPATIA HUYU MTU.

Angekuwa hana uhakika wa alichonacho, asingeweza kukitoa... Huwezi kutoa kitu ambacho huna uhakika kuwa unacho.

Hii inadhihirisha wazi, si kwamba alijulia muda ule kwamba anao UZIMA NDANI YAKE WA KUMGAWIA HUYU KIWETE.

Hii inadhihirisha kwamba, Petro alikuwa na aina ya maisha inayotilia mkazo alichonacho kiasi kwamba JAPO KILIKUWA HAKIONEKANI KWA NJE LAKINI KILIKUWA HALISI KWAKE KIASI CHA KUWEZA KUKIGAWA KWA WENGINE... KIASI CHA KUWEZA KUKIDHIHIRISHA NJE (He was able to materialize his inner potential).

Anza kuwa na maisha yanayokipalilia kile ulichonacho (your potential, talent gift etc) hata kama watu bado hawajajua unacho (wasichokijua watu kwamba unacho).

Baada ya Petro kudhihirisha alichonacho ndani yake, HATUONI TENA MAHALI PENGINE AKISEMA SINA FEDHA WALA DHAHABU, ninaamini baada ya TUKIO HILI LA KUDHIHIRISHA ALICHOBEBA NDANI, NDIO ULIKUWA MWISHO WA KUTOKUWA NA FEDHA NA DHAHABU.

Ukifanikiwa KUDHIHIRISHA ULICHO NACHO KWA UKAMILIFU, HICHO ULICHO NACHO NDANI KITAVUTA FEDHA NA DHAHABU KWENYE MAISHA YAKO. KITAWAVUTA WATU SAHIHI KWENYE MAISHA YAKO.

Nijisemee mimi, Ninaweza nisiwe na fedha au dhahabu za kuwapatia watu au mtu, lakini NILICHO NACHO NI HALISI MNO KULIKO FEDHA AU DHAHABU. KILA ALIYETAYARI KUPOKEA NINAWEZA KUMGAWIA, NA NINA UHAKIKA KUWA NINACHO. TUKIKAA WOTE MASAA KADHAA UTAKIONA KWA UHALISIA, UNAWEZA USIONDOKE NA HATA SHILINGI MOJA LAKINI KWA HAKIKA UTAONA UMEONDOKA NA KITU, UMEONDOKA NA UZIMA, NGUVU MPYA, MATUMAINI MAPYA. SABABU NDANI YANGU NINABEBA UZIMA, NINABEBA MAISHA, NINAMBEBA YESU HALISI ANAYEWEZA KUJIDHIHIRISHA (JESUS WHO CAN BE MATERIALIZED), SIO TU YESU ALIYEANDIKWA BALI ALIYE HAI.

Ninabeba UZIMA, Hata kwenye ujumbe huu kuna uzima kwa kila aliyetayari kuupokea.

Kitakachokutambulisha ni ULICHO NACHO NA SI USICHONACHO.

GEUZA MTAZAMO WAKO NA UTAONA KANUNI HII YA NENO LA MUNGU IKIFANYA KAZI KWAKO.

USICHOKUWA NACHO HAKIKUSAIDII, USIHANGAIKE NACHO, BADALA YAKE KIENDELEZE ULICHONACHO NA UWAGAWIE WENGINE PIA, UKIFANYA HIVYO HAUTABAKI ULIVYO.

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

Umebarikiwa

~Na. Mwl. Francis M. Langula

(+255754711247)

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!