Text

Usimfikirie Mtu Mwingine, ni Wewe Utakayetatua Hiyo Changamoto Unayoiona

1 views 1 day ago

Yoshua1:5-6 SUV

"Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. 6Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa."

Ukiangalia kwa makini maneno hayo kwenye mstari wa 6 

"maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii

utagundua Yoshua alikuwa akifikiria kuwa inawezekana kuna mtu mwingine aliyepewa kazi hiyo ya kuwarithisha Israel nchi ya Kanaani.

Ukisoma kuanzia mstari wa kwanza utagundua kuwa, inaonekana Yoshua hakuwa anajua kama Musa ameshakufa tayari, kwa hiyo Mungu ndio alikuwa anampasha habari, na aliposikia habari hizo inawezekana ndio akaanza kujiuliza maswali hayo ya msingi, kwamba, je ni nani ataifanya kazi ya Musa kuwarithisha Israel nchi? na katika mstari wa 6 ndipo Mungu akamjibu kuwa ni yeye ataifanya kazi hiyo!

Ni wazi kabisa Mungu alikuwa anajibu swali lake kwamba, Sasa Musa ameshakufa, sijui ni nani anayetakiwa kuturithisha nchi hii!!

Naamini walikuwepo wengi Israel, lakini sio wote waliokuwa wanawaza juu ya jambo au swali hilo, kwamba Musa amekufa sasa ni nani ataifanya kazi hiyo? Wengine waliona kawaida tu.

Kwa hiyo, Ilihali unapata shida kwamba jambo hili litafanywa na nani, basi ujue kwamba hicho ni kiashiria kwamba wewe ndio mtu sahihi wa kulifanya au una wajibu wa kufanya ili kutatua tatizo,  acha kumfikiria mwingine, UWE HODARI NA MOYO WA USHUJAA, chukua hatua!

Mara nyingi Mungu akikutaka ufanye kitu anakuruhusu kuona mapungufu!

Sio lazima kwamba huo upungufu au uhitaji, kila mtu anauona, kuna wengine wanaona kawaida tu, kama wewe unauona ujue una wajibu wa kufanya kuhakikisha unashughulikia upungufu huo!

Sasa kosa letu ni pale tunapoona upungufu na badala ya kufikiria kutoa suluhisho tunafikiria kulaumu wengine!

Nina uhakika kuna wengine waliona kweli Musa amekufa, lakini hilo swali halikuwasumbua!

Ni Gideoni pekee ambaye pamoja na kwamba alikuwa amejificha shinikizoni lakini muda wote alikuwa anaona kuna jambo haliko sawa mpaka akawa anasema "Yuko wapi Mungu tunayesikia habari zake kwamba aliwatendea baba zetu"? - Malika alipomtokea alimwambia enenda kwa uwezo wako huo!

“Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa BWANA yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye BWANA, aliyetuleta huku kutoka Misri?* Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. BWANA akamtazama, akasema, *Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?” Waamuzi 6:13-14 SUV

Uwezo wa kugundua kwamba hapa kuna kitu hakipo sawa na Mungu anaweza kabisa kufanya kitu ni mtaji tosha wa kuchukua nao hatua na hali hiyo ikabadilika!

NYUMA YA UWEZO WA KUGUNDUA TATIZO KUNA UWEZO WA KUTATUA TATIZO PIA, SHIDA NI KWAMBA TUNAISHIA HAPO KWENYE KULIONA NA KULIGUNDUA TATIZO TU!

Kuna watu tukiona upungufu tunaanza kuukosoa badala ya kufikiria jinsi gani tutatoa mchango wetu katika kutatua!

Mungu anamwambia Joshua, USIMFIKIRIE MTU MWINGINE, NI WEWE UTAKAYEWARITHISHA WATU HAWA NCHI HII!

Ni wewe utakayehusika kutatua huo upungufu unaouona au hilo tatizo unaloliona, acha kunyooshea watu vidole, chukua hatua sahihi!

Daudi ndiye aligundua kwamba kitendo cha Gorlathi kuwatukana majeshi ya Mungu hakiko sahihi, na ni yeye (Goliathi) aliyeshughulika ipasavyo!

“Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?" 1 Samweli 17:26 SUV

KAMA UKIWEZA KULIONA TATIZO, ANGALIA VIZURI, UTALIONA NA JIBU LA TATIZO LIKO NDANI YAKO!

Daniel aliweza kuona kwamba, hapa kuna shida mahali ndio maana Israel wamekaa utumwani kupita Muda ulioamriwa, na yeye mwenyewe alisababisha suluhisho kwa maombi yake!

KILA ANAYEWEZA KUONA TATIZO AKIANGALIA VIZURI ATAONA NA JIBU!

KAMA UNA UWEZO WA KUONA WATESI, ANGALIA VIZURI UTAIONA NA MEZA IMEANDALIWA!

“Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu.” Zaburi 23:5 SUV

KAMA UNAWEZA KUONA WENGI WAKUPINGAO, ANGALIA VIZURI UTAUONA NA MLANGO MKUBWA UMEFUNGULIWA MBELE YAKO PIA!

“kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.” 1 Wakorintho 16:9 SUV

UKIMUONA GOLIATHI ANGALIA VIZURI, UTAGUNDUA KOMBEO LIPO, MAWE YAPO, NA USHUHUDA WA KUMUUA DUBU NA SIMBA UPO; chukua hatua mshughulikie maana MUNGU YU PAMOJA NAWE! 

MUNGU YUKO PAMOJA NAWE, chukua hatua mpendwa! Usiishie kulia na kulalamika unapoona au kukutana na changamoto!

NI WEWE, SIO MWINGINE NI WEWE, KWA HIYO "Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa."

 

#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili

Umebarikiwa

~Na. Mwl. Francis M. Langula

(+255754711247)

Comments (0)
Login to leave a comment.

No comments yet. Be the first to comment!