Usipuuze Wazo la Mungu Kwa Sababu ya Uchache wa Ulivyonavyo, Aliyekupa Wazo Anajua Cha Kufanya
Yohana 6:5- 11
"Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula? Na hilo alilinena ili kumjaribu; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda. Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu. Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa? Yesu akasema, Waketisheni watu. Na mahali pale palikuwa na majani tele. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka."
Bwana Asifiwe wana wa Mungu!
Roho Mtakatifu ameyaweka maneno hayo niliyonuku, ndani yangu naamini kuna jambo kubwa la kujifunza hapo.
Yesu aliona mkutano mkuu ukimwendea, Neno la Mungu linasema, walikuwa WANAUME ELFU TANO.
Mara nyingi kama si mara zote, wanawake huwa wanakuwa wengi kuliko wanaume kwenye mikutano ya aina hii, kwa hiyo, kama wanaume walikuwa elfu 5, inawezekana kabisa huu mkutano ulikuwa na watu ZAIDI YA ELFU KUMI.
Kwa hiyo, ulikuwa ni mkutano mkubwa sana wa watu.
Neno la Mungu linasema "Basi Yesu alipoinua macho yake akaona mkutano mkuu wanakuja kwake, alimwambia Filipo, Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?"
Kwa hiyo, Yesu mwenyewe NDIYE MUASISI WA WAZO LA KUWALISHA WATU HAWA ZAIDI YA ELFU 10, na sio wanafunzi waliolianzisha wazo hilo.
Ukifuatilia maandiko haya kwenye kitabu cha Marko 6:32-44, Mathayo 14:13 - 21 na Luka 9:10-17 (ambao, pia wameiandika habari hii) utagundua, wanafunzi walitaka watu watawanyike wakatafute chakula, lakini YESU NDIYE ALILETA WAZO LA KUWALISHA.
Hawa watu, hawakwenda kwa Yesu kwa lengo la kula, Walienda kufundishwa, na kuponywa magonjwa yao, lakini pia HALIKUWA KWENYE MAWAZO YA WANAFUNZI KABISA, swala la KUWALISHA HAWA WATU.
Kwa maelezo hayo, ni wazi kabisa, lilikuwa ni WAZO LA YESU, KUWALISHA WATU ELFU 10, na sio la wanafunzi, au kwa lugha nyingine, ILIKUWA NI AGENDA YA YESU na sio ya wanafunzi.
Sasa kama ilikuwa ni agenda ya Yesu, maana yake, Yeye mwenyewe ndiye alikuwa wa kuhakikisha inafanyika kikamilifu, kazi kubwa ya wanafunzi ilikuwa ni kulikubali au kulipokea HILO WAZO na kurudi kwa YESU kuona atatoa MAELEKEZO GANI au MBINU GANI katika kulitimiza WAZO LAKE.
Ndio maana Neno la Mungu tulilonukuu linasema "Na hilo [Yesu] alilinena ili kumjaribu [Filipo]; kwa maana alijua mwenyewe atakalotenda"
Kwa sababu ni WAZO LAKE, ALIKUWA ANAJUA KABISA NI NINI ATAKACHOFANYA KULITIMIZA.
Sasa huo ni upande wa kwanza wa kile ninachotaka tukiangalie.
--Upande wa pili ni wa FILIPO na ANDREA.
Yesu akaamua amshirikishe FILIPO lile WAZO na baadaye, Andrea naye akashiriki kwa kutoa maoni yake kwenye WAZO LA YESU KUWALISHA WATU ZAIDI YA ELFU KUMI.
Neno la Mungu linasema, "Filipo akamjibu, Mikate ya dinari mia mbili haiwatoshi, kila mmoja apate kidogo tu."
Filipo alilisikia wazo la Yesu, lakini hali ya uchumi waliyokuwa nayo ikamfanya alikatae (asilipokee) au kwa lugha nyingine, aone haliwezekani... Kimsingi, hata hakulielewa vizuri.
Kwa nini nasema alilikataa au inawezekana hata hakulielewa?
Yesu hakuuliza kwamba "Je tuna pesa za kutosha kununua mikate ya hawa watu wapate kula?" bali aliuliza "Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?"
Kwenye swali la Yesu, PESA HAIKUWA TATIZO KABISA, swali lilikuwa "Tununue wapi mikate" Lakini, Filipo akaangalia MFUKO WAO, AKAONA UNA DINARI MIA MBILI TU, AMBAZO HAZITOSHI KABISA kutekeleza WAZO LA YESU.
KITU ALICHOSEMA FILIPO NI HALISI LAKINI, SIO "CONCERN" YA YESU WALA HAKIKUWA KIZUIZI KWA WAZO LA YESU.
Ukisoma maandiko (Mathayo 20:2-13) utagundua kwamba, dinari moja ilikuwa ni malipo ya kawaida ya siku moja kwa mtu (au mshahara wa kibarua wa siku) - the ordinary pay for a day's wages.
Tukienda kimahesabu ya sasa hivi, kibarua wa kawaida anaweza akawa analipwa kati ya Shilingi za Kitanzania elfu 5 mpaka labda elfu 15 kwa siku (haya ni makadirio tu kwa lengo la kujaribu kufananisha mazingira ya kina Filipo na tulionayo sasa ili tuweze KUJIFUNZA JAMBO LA KUTUFAA KIZAZI HIKI).
Kwa hiyo, tukichukua kwa kadirio la kati, dinari moja ya kipindi kile inaweza kuwa sawa na elfu 10 kwa sasa, hii itamaanisha DINARI 200 WALIZOKUWA NAZO NI SAWA NA Shilingi MILIONI 2 (Tsh. 2,000,000/=), haya ni makadirio tu, inaweza isiwe sahihi sana.
Idadi ya watu waliotakiwa kula walikuwa zaidi ya elfu 10, kwa hiyo kwa mgawanyo tu wa kawaida wa pesa iliyokuwepo, KILA MTU ANGEPATA pungufu ya Tsh. 200/= ambayo kwa namna yoyote ile pesa hiyo isingetosha kwa chakula aina yoyote.
Kwa hiyo, kimahesabu, FILIPO ALIKUWA SAHIHI KABISA, lakini alikuwa "OFF POINT", kwa maana kwamba, YESU HAKUMTAKA AMPIGIE MAHESABU YA PESA WALIYONAYO, YESU ALITAKA TU KUJUA MIKATE INAPATIKANA WAPI?
Mungu akikupa wazo lake, HATAKI UPIGE MAHESABU YA PESA ULIZONAZO ILI KUTIMIZA WAZO LAKE.
Yesu aliuliza hivi "Tununue wapi mikate, ili hawa wapate kula?"
Ukifuatilia kwa umakini andiko hilo, UTAGUNDUA KWAMBA, SWALA LA YESU HAPA LILIKUWA NI KUPATA MIKATE TU, BILA KUJALI KABISA IDADI YA MIKATE, VINGINEVYO ANGEWEZA KUSEMA "TUPATE WAPI MIKATE YA KUTOSHA WATU HAWA KULA"?
Yesu hakuuliza, tupate wapi mikate ya kutosha.
Labda nielezee kidogo hapa; kimsingi, kwenye tukio hili, kwa hali ya kawaida kabisa kulikuwa na MASWALA MAKUBWA MAWILI YAKUYASHUGHULIKIA (Two basic issues to address);
Swala la kwanza, ni KUWA NA PESA YA KUTOSHA KUNUNUA MIKATE (Having sufficient money to buy breads), ambayo ndilo FILIPO ALILIWAZA, lakini swala la pili, ni KUPATA MIKATE YA KUWATOSHA WATU ZAIDI YA ELFU 10 (Having sufficient supply or a supplier(s) to buy this much bread).
Pamoja na kwamba hakukuwa na pesa ya kutosha lakini, kwa hali ya kawaida, hata kama una pesa za kutosha, huwezi kupata chakula cha watu wengi kiasi hicho bila kuweka order na iandaliwe kwa muda wa kutosha.
Lakini, NINACHOTAKA UONE HAPO ni kwamba, SWALI LA YESU HALIKUWA LINAJALI haya maswala mawili, yaani UWEPO WA PESA, WALA UPATIKANAJI WA MIKATE (WINGI WA MIKATE), swali la Yesu LILIKUWA LINATAKA MKATE AU MIKATE TU, BILA KUJALI WINGI AU IDADI YA MIKATE.
Nini tunaweza kujifunza kutoka kwenye ufafanuzi niliotoa hapo juu?
Hiki ndicho kinachotokea sana hata kwenye maisha yetu.
Neno la Mungu linasema katika Yeremia 29:11 "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho."
Kama vile Yesu alivyokuwa anawawazia mawazo mazuri hawa makutano bila hata wao kujua, ndivyo Mungu hutuwazia mawazo ya amani (mawazo ya kutufanikisha).
Na kama vile Yesu alivyolileta wazo lake kwa wanafunzi wake, Ndivyo hivyo Mungu au Roho Mtakatifu HUTULETEA MAWAZO YAKE MAZURI NDANI YETU, ili tuyafanyie kazi na yatufanikishe.
Wazo la Mungu (idea) linapotujia, huwa halijali UWEZO TULIONAO WAKATI HUO ILI KULITIMIZA HILO WAZO.
Kwa upande mwingine, watu wengi tukilipokea wazo la Mungu (laweza kuwa la Biashara, huduma, kununua kiwanja, kuanza mradi fulani nk), TUNAANZA KUANGALIA UWEZO WETU KATIKA KULITEKELEZA HILO WAZO, TUNAANZA KUANGALIA VYANZO VYETU (OUR RESOURCES), TUNAANGALIA PESA TULIYO NAYO, HALI ZA UKOO NA FAMILIA ZETU, tunaangalia UCHUMI wa eneo tulipo, na mwisho TUNAJIKUTA TUNALIKATAA WAZO LA MUNGU.
Lakini, ukweli ni kwamba, MUNGU ANAPOKULETEA WAZO, ANAJUA YEYE MWENYEWE ATAKACHOFANYA ILI KUKUSAIDIA LILE WAZO LIFANIKIWE.
Wajibu wetu wa kwanza, NI KULIPOKEA WAZO LA MUNGU BILA KUJALI HALI TULIYO NAYO.
Neno linasema, Yesu alipolileta wazo lake kwa wanafunzi wake ".....alijua mwenyewe atakalotenda."
Mungu akikupatia wazo, anajua mwenyewe njia ya kufanya litimie, WEWE LIPOKEE, LIANDIKE, LIOMBEE, ANZA KULIFUATILIA, CHUKUA HATUA NDOGO YA MWANZO* UNAYOIWEZA, MENGINE MUNGU ATAYAFANIKISHA.
Kwa maandiko tuliyonukuhu hapo juu, na yale niliyoyataja kutoka kwa waandishi wengine (Marko, Luka na Mathayo) walioandika tukio hili, inaonekana wazi kabisa, Wazo la Yesu liliwafikia wanafunzi wote, japo aliyelengwa kwanza ni Filipo (sababu Yesu alimtaja kabisa kwa mujibu wa uandishi wa Yohana) lakini, inaonekana kabisa wazo hili liliwafikia wote.
Kwenye ufafanuzi nilioweka juu, tumeona kwa undani namna Filipo alivyolipokea WAZO LA YESU, lakini pia kati ya wanafunzi 11 waliobaki, Andrea naye alijieleza namna alivyolipokea WAZO LA YESU, wale wengine 10 hatuoni wakisema chochote.
Nataka tujifunze kitu kutoka kwa muitikio wa Andrea kwa WAZO LA YESU LA KULISHA WATU ELFU 10.
Maandiko yanasema "Wanafunzi wake mmojawapo, Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia, Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?"
Ni kama vile Andrea ALIWEZA KULIDAKA VIZURI SANA WAZO LA YESU.
Mstari huo hapo juu unasema Andrea akasema "Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili, lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?"
Maneno hayo ya Andrea yana sehemu mbili, sehemu ya kwanza (Yupo hapa mtoto, yuna mikate mitano ya shayiri na samaki wawili) inalipokea wazo la Yesu, na sehemu ya pili (lakini hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?) inaanza kulionea shaka wazo la Yesu na KULIKATAA.
Andrea alipokea wazo vizuri, lakini akaanza kuangalia hali iliyowazunguka, akaanza kuangalia uchache wa walivyonavyo mkononi (resources), akaanza kuangalia upungufu wa mikate.
Ukweli ni kwamba, MLETA WAZO ALIKUWA ANAJUA ATAKACHOKIFANYA.
Jibu la kwanza la Andrea ndio lilikuwa sahihi na ndio lilikuwa la Ki-Mungu au lenye imani, kwa sababu kwa hali ya kawaida kabisa, mtu hawezi akakuambia nataka chakula cha watu elfu 10 halafu ukamwambia kuna samaki wa wawili na mikate mitano, utaonekana kama haujui kufikiri "reason" sawasawa au jibu lako HALINA MANTIKI, HII NI WAZI KWAMBA ANDREA ALIDAKA WAZO KIMUNGU LA YESU, ambalo lilikuwa JUU YA FAHAMU (REASONING) ZA KAWAIDA ZA KIBINADAMU.
Mungu anapotuletea WAZO, haitaji KWANZA REASONING ZETU (sio lazima liwe na mantiki kwanza), ANAHITAJI KWANZA TULIPOKEE. Na hapa ndipo wengi tunapofeli katika utekelezaji wa MAWAZO YA MUNGU.
Mungu anapotuletea wazo, haangalii kwanza uwezo wetu tulionao sasa katika kulitimiza hilo wazo, YEYE MWENYEWE ANAJUA ATAKACHOFANYA TUKILIPOKEA.
Lakini pia, kingine kinachoonyesha alidaka wazo la Yesu, na Jibu lake la kwanza lilikuwa ni jibu la KiMungu, ni namna Yesu alivyoitikia baada ya Jibu la Andrea.
Yesu aliitikia JIBU LA KWANZA LA ANDREA na sio la pili.
Mara baada ya jibu la Andrea, maandiko yanasema "Yesu akasema, Waketisheni watu...... Basi watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao. Basi Yesu akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri walivyotaka." Yohana 6:10-11
Yesu alitaka Filipo na wanafunzi wake WALIPOKEE wazo, halafu, WAMPATIE ALICHOKUWA ANATAKA KUTOKA KWAO (yaani wamkabidhi mikate na samaki) bila kujali ni kiasi gani, bila kujali vinatosha au la, halafu WASIKILIZE MAELEKEZO YAKE, kwa sababu YEYE ANAJUA ANACHOTAKA KUFANYA.
Mungu akikupa wazo (la biashara, mradi, husuma, kununua kitu, kusoma nk), KWANZA LIPOKEE, LIANDIKE, LIFUATILIE KWA UKARIBU (Fanya analysis za kutosha), HUKU UKILIOMBEA NA KURUDI KWAKE MARA KWA MARA (KWA NJIA YA MAOMBI NA KUMUULIZA ROHO MTAKATIFU) ILI AKUPATIE MAELEKEZO YA HATUA ZA KUFUATA NA UANZE KUTEKELEZA HATUA NDOGO UNAYOWEZA, usiogope hata kama huna pesa, huna mtaji, huna uwezo kulitimiza, wewe lipokee na ulifanyie kazi, ALIYEKUPA WAZO ANAJUA ATAKACHOFANYA, ONYESHA USHIRIKIANO.
USIPUUZE WAZO LA MUNGU KWA SABABU YA UCHACHE WA ULIVYONAVYO, ALIYEKUPA WAZO ANAJUA CHA KUFANYA
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author