Yesu Alichukua Magonjwa na Madhaifu Yote Bila Kujali Chanzo Chake
Mathayo 8:17
"Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu."
Ndani yangu Roho Mtakatifu ameliweka Neno hili kwa namna ya kipekee kabisa.
Andiko hili ni sawa kabisa na hundi iliyosainiwa na iko wazi kwenye kiasi cha pesa, yaani anayeipokea ndiye anajaza mwenyewe kiasi cha pesa anachotaka.
Neno lina sema, ALIUTWAA UDHAIFU WETU NA KUYACHUKUA MAGONJWA YETU na baada ya hapo linatuachia sisi tujaze ni Udhaifu gani na ni magonjwa gani.
Neno haliongelei UDHAIFU GANI WALA MAGONJWA GAN, sisi ndio tunapaswa kutaja udhaifu na magonjwa.
Ukifuatilia tafsiri mbalimbali, Neno UDHAIFU linamaanisha Maumivu, au Hali yoyote ya afya mbaya au Upungufu wa nguvu.
Na neno MAGONJWA ni kama linavyomaanisha au ni hali ya kuwa mgonjwa eneo lolote la mwili au nafsi.
Lakini pia, Ukifuatilia utagundua viko vyanzo mbalimbali vya UDHAIFU na MAGONJWA, vingine ni vyanzo vya kiroho na vingine ni vya kisayansi na vingine ni vya kimazingira na vya kibinadamu.
Kuna magonjwa na madhaifu yanasababishwa na uzembe wa mtu binafsi au watu wake wa karibu, yapo yanayosababishwa na dhambi ya mtu, yapo magonjwa yanayotokana na sababu za kisayansi, mengine sababu za kimazingira au hali ya hewa, lakini ni wazi kabisa yapo magonjwa yanayosababishwa na wachawi na pia yanayosababishwa na mapepo au nguvu za giza. Hivi ni vyanzo kadhaa ambavyo tunaweza kuviona hata kwenye maandiko.
Luka 10:3,9,17-18 “Enendeni, angalieni, nawatuma kama wana kondoo kati ya mbwa-mwitu. waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia. Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.”
Mathayo 8:16 “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,”
Neno la Mungu linasema, Yesu, bila kujali chanzo cha UGONJWA AU UDHAIFU, "Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu"
Neno hilo ni sawa na swali ambalo halina jibu moja, yaani jibu lolote la ugonjwa au udhaifu ni sahihi. Kwenye "kuyachukua magonjwa" ukiweka ugonjwa mmoja na mengine ukayaacha usiyaweke utakuwa umejibu sahihi.Lakini pia ukiyaweka yote pia umejibu kwa usahihi zaidi. Kila ugonjwa unafit hapo.
Ukiacha baadhi ya magonjwa sababu ya chanzo chake uko sahihi, ukiweka magonjwa yote bila kujali chanzo uko sahihi zaidi.
Kuna watu wameshindwa kusimama na kupokea uzima wao sababu ya kufikiri chanzo cha ugonjwa au udhaifu. Wengine kwa sababu magonjwa yao yamesababishwa na uzembe wao au dhambi zao basi wanajitoa kwenye orodha ya wanaofaidika na andiko hili. Wanasahau kwamba, Andiko hili halizingumzii chanzo linazungumzia matokeo ya KAZI NZURI YA YESU.
Kwa nini chanzo cha ugonjwa sio muhimu hapa?
Jibu la moja kwa moja ni kwamba, MUASISI WA MAGONJWA YOTE NI SHETANI. Yaani Ukienda nyuma ya chanzo chochote UTAMKUTA SHETANI HAPO.
Ninachomaanisha ni kwamba, kabla ya uzembe, kabla ya vyanzo vya kisayansi, kabla ya magonjwa ya kipepo au kichawi au ya kurithi, kabla ya yote hayo, shetani ndiye muasisi wa magonjwa, dhambi ilipoingia ndipo na magonjwa yaliingia hii ni kabla hata ya sayansi kuingia, hii ni pale Edeni.
Kwa hiyo, Yesu hakuja kushughulika na kingine ISIPOKUWA ALIKUJA KUZIVUNJA KAZI ZA IBILISI ambazo ndani ya hizo kuna DHAMBI ZOTE NA MAGONJWA YOTE.
1 Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.”
Yesu alidhihirishwa ili azivunje kazi za ibilisi ambazo ni dhambi na magonjwa, pamoja na zingine.
Matendo ya Mitume 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”
Yesu aliponya WOTE WALIOONEWA NA IBILISI, kwa hiyo kwenye kila ugonjwa kuna MKONO WA IBILISI.
Ukitaka kuyashughulikia magonjwa vizuri, yashughulikie kama unamshughulikia SHETANI.
Sasa, fundisho hili halimaanishi tusiwe waangalifu linapokuja suala la afya zetu, bali ninaweka msisitizo kwamba tusimvumilie "Shetani" anayeitwa ugonjwa kwa kisingizio cha chanzo chake na wakati YESU ALISHASHUGHULIKA NA MAGONJWA NA MDHAIFU YOTE BILA KUJALI CHANZO CHAKE.
Kama chanzo ni dhambi, Yesu alishughulika na dhambi na magonjwa yanayoambatana na dhambi pia.
Yesu ameyachukua magonjwa Yetu bila kujali chanzo chake.
Na kama AMEYACHUKUA, MIMI SINA, KAMA YAKO KWAKE HAYAWEZI KUWA KWANGU.
If he took I don't and I can't have even one.
#UponyajiWaKiMunguKwaWoteWenyeMwili
#Umebarikiwa
~Na. Mwl. Francis M. Langula
(+255754711247)
Mwl. Francis Langula
Author